Simba yafufua kesi ya Lawi

BAADA ya tetesi kuibuka kuwa beki wa kati wa Coastal Union, Lameck Lawi anatajwa kujiandaa kutua Yanga, mabosi wa Simba wameamua kuifufua upya kesi dhidi ya mchezaji huyo katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kama mnakumbuka, Lawi alikuwa mchezaji wa kwanza kutambulishwa na Simba dirisha lililopita kabla ya Coastal kuibuka na kudai biashara juu ya mchezaji huyo ilishakufa kwa kushindwa kutimiza masharti ya kutoa dau la mauzo ya beki huyo, kisha jamaa akaenda zake Ubelgiji kutesti zali la kucheza soka la kulipwa.

Simba ilikimbilia TFF kwa kufungua kesi katika Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji na ikaonekana walizingua wenyewe na Lawi kubakishwa Coastal na alipokwama kutua KAA Gent alirejea kwa Wagosi na kuendelea kukipiga kama kawaida, ila hivi karibuni zikaibuka tetesi Yanga inamnyemelea.

Kitendo cha beki huyo kuhusishwa na Yanga, imewaamsha upya mabosi wa Msimbazi na kuamua kukimbilia TFF kuifufua kesi yao na taarifa zinasema kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa leo Alhamisi kabla dirisha dogo la usajili halijafunguliwa na kumwezeshja Lawi kutua Jangwani.

Akizungumza na Mwanaspoti jana mchana, Mwenyekiti wa Kamati Sheria na Hadhi za Wachezaji, Said Soud alisema amesikia taarifa za kukutana ili  kujadili sakata hilo linalomhusu Lawi na Simba.

“Nimsikia taarifa hizo juu kwa juu, kutakuwa na kikao kesho (leo) kwa ajili ya kujadili sakata linalomhusu mchezaji Lawi na Simba,” alisema Soud, ambaye hatakuwepo sehemu ya wajumbe wa kuijadili kesho kama alivyofanya mwanzo kwa kilichoelezwa yeye ni mwanachama wa Coastal.

Related Posts