Wananchi walalama gharama kubwa huduma za kisheria

Musoma. Baadhi ya wakazi wa Musoma, mkoani Mara, wamesema kuwa gharama kubwa za huduma za wanasheria ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wengi kushindwa kupata haki zao kisheria, hali inayochangia kuibuka kwa migogoro mbalimbali, ikiwemo ya ardhi katika jamii.

Wakizungumza leo Jumatano, Desemba 11, 2024, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria ijulikanayo kama Mama Samia Legal Aid mjini Musoma, wakazi hao wamezitaka taasisi na wadau mbalimbali kushirikiana na serikali ili kuhakikisha utoaji wa huduma za kisheria unaendelea katika maeneo yote nchini.

Sadiki Hussein amesema wananchi wengi wanashindwa kumudu gharama za mawakili na wanasheria kutokana na hali ya maisha ilivyo hivyo kubaki na changamoto zao zinazohitaji utatuzi wa kisheria hali ambayo kwa namna moja ama nyingine imekuwa ikidumaza ustawi wa wananachi kijamii na kimaendeleo.

“Kumuona wakili au mwanasheria gharama ya chini kabisa ni Sh10,000 hapo bado hajakubali kukuwakilisha mahakamani ambapo kwa wale wenye bei ndogo ili asimamie kesi yako atakudai si chini ya Sh1 milioni  sasa gharama hiyo kwa mwananchi ambaye hana hata uhakika wa milo mitatu kwa siku unafikiri anaweza kumudu?,” amehoji Hussein.

Anna Mtatiro amesema hali ni mbaya zaidi kwa wakazi wa maeneo ya vijijini ambako hakuna huduma za kisheria hivyo kwa wale wanaohitaji huduma za wanasheria wanalazimika kusafiri hadi mijini ambapo kuna huduma hizo.

“Hapo inategemana na kijiji unachotoka kuna maeneo hauwezi kufika mjini na kurudi siku hiyo hiyo hivyo utalazimika kulala ili upate huduma sasa ukiangalia hizo gharama mtu unakata tamaa na kuamua kubaki na shida zako,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, wamesema kuna haja ya wadau kuunga mkono jitihada za serikali kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinapatikana kwa watu wote bila kujali hali zao za kiuchumi.

“Bahati mbaya suala la sheria haliangalii wewe masikini au tajiri kwasababu tunaambiwa wote tuna haki sawa mbele ya sheria lakini kiuhalisia maskini ni vigumu kupata hiyo haki kwasababu hawezi kumudu hizo gharama,” amesema  Dominic Mugyabuso.

Mugyabuso ameipongeza Serikali kwa kubuni kampeni hiyo, huku akisema ipo haja ya kampeni hiyo kuwa endelevu.

Awali, akisoma hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dk Halfan Haule ameiomba serikali kufanya maboresho ya namna ya kushughulikia migogoro ya.

Amesema umefika wakati sasa wa kuziruhusu mahakama kutumika kuamua migogoro badala ya mabaraza ya ardhi ambayo pamoja na mambo mengine, yameshindwa kutoa uamuzi wa migogoro hiyo kwa wakati kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo kukosekana kwa mabaraza.

Mtambi amesema, Mkoa wa Mara unakabiliwa na migogoro mingi ya ardhi kutokana na sababu nyingi ikiwemo ya kukosekana kwa utatuzi wa migogoro hiyo kwa njia za kisheria.

Amesema hali hiyo inasababishwa na kutokuwepo kwa mabaraza ya ardhi katika maeneo mengi ambayo yalikuwa na mamlaka ya kutoa uamuzi wa kisheria.

“Migogoro ya ardhi ni mingi sana, hii changamoto ni vema ikafanyiwa kazi, kuna mlolongo mrefu sana katika kupata uamuzi wa kisheria, mfano hapa Mara kuna wilaya kama Rorya na Butiama hazina mabaraza hayo hivyo wananchi wanalazimika kusafiri hadi Musoma au Tarime kupata huduma na hii inapelekea watumie gharama kubwa na muda mwingi kutafuta haki yao,” amesema.

Amesema hali hiyo nawakatisha tamaa wananchi hasa wa wanapotafuta ufumbuzi wa migogoro kisheria.

Akizungumzia ombi hilo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini amesema tayari serikali imeziagiza Wizara ya Katiba na Sheria na ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Mkazi kukutana ili kuhuisha mfumo wa mashauri ya ardhi ili yawezekana kushughulikiwa  kimahakama.

“Ni kweli sekta ya mahakama imeimarisha na kuboresha sana huduma zake na tayari serikali imeliona hilo la mashauri ya ardhi, kuchukua muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya ukosefu wa mabaraza katika maeneo mengi,” amesema.

Hata hivyo amesema mchakato unaendelea ili yaweze kufanyiwa kazi kwa mfumo wa kimahakama.

Akizungumzia kampeni ya msaada wa kisheria,  Sagini amesema inalenga kuwapatia elimu wananchi na juu ya upatikanaji wa haki mbalimbali  kisheria bila malipo.

Amesema kampeni hiyo ikifanikiwa itaimarisha utoaji wa huduma, ushauri wa kisheria kwa waathirika wa masualanya ukatili wa kijinsia.

Mjumbe wa Bodi ya Msaada wa kisheria msaada wa kisheria, Lucas Malunde ameipongeza wizara ya Katiba na Sheria kwa kampeni hiyo.

Amesema ni nyenzo muhimu katika kuhimiza na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wale wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili.

Related Posts