Historia nyingine yaandikwa utekelezaji miradi ya umeme

Dodoma. Tanzania imeandika historia nyingine ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya umeme baada ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kuzindua utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400, kutoka Chalinze hadi Dodoma na upanuzi  wa vituo vya kupoza umeme vya  kilovoti 400 Chalinze – Pwani na Zuzu – Dodoma.

Mradi huo wa umeme uliozinduliwa leo Jumatano Desemba 11, 2024 utawezesha  umeme wote unaozalishwa katika mradi wa kuzalisha umeme wa JNHPP, kufika katika maeneo yote ya mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini, Kati na Magharibi, kwenye migodi na viwanda. Lengo likiwa ni kuimarisha biashara ya umeme Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dodoma, Dk Biteko amesema kutekelezwa kwa mradi huo ni miongoni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa Wizara ya Nishati kuwa iendelee kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ilete tija kwa Taifa.

Dk Biteko amesema kutokana na jitihada hizo zinazofanywa na Serikali kuendeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji

umeme, imeifanya Tanzania kuwa kinara barani Afrika katika usambazaji wa umeme kwa wananchi na hii ni kutokana na takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia.

Amesema Serikali imeendelea na jitihada za kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme nchini kwa kuongeza uwezo wa mitambo ya kufua nishati hiyo  inayozalisha

“Mahitaji ya juu ya umeme nchini kwa sasa yamefikia megawati 1,888.72 na mahitaji hayo hayajawahi kufikiwa tangu nchi ipate uhuru,  hii ikimaanisha kuwa uchumi unazidi kukua kutokana na kuongezeka kwa shughuli za maendeleo,” amesema Dk Biteko.

Amesema kuimarika kwa uzalishaji huo  kumechangiwa na kuanza kwa uzalishaji katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 ambao hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 99.6 na jumla ya megawati 1,175 za umeme zinazalishwa na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.

Katika hatua nyingine Dk Biteko amekemea wahujumu wa miundombinu ya umeme ambao amesema wanarudisha nyuma uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.

Akizungumzia makandarasi wa mradi huo, Kampuni ya TBEA kutoka China, amewataka wahakikishe mradi unakamilika kwa wakati kama mkataba unavyoonyesha.

Pia ametumia hafla hiyo kuwakumbusha viongozi na wananchi kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Amesema Serikali imetoa ruzuku kwa

mitungi ya gesi zaidi ya 400,000 itakayouzwa kwa nusu gharama ya bei ya soko na  inasambazwa katika mikoa yote Tanzania Bara.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema mradi huo ni muhimu kwa nchi kwa kuwa inategemewa kuimarisha hali ya umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika kupitia miradi ya uzalishaji na usafirishaji umeme ambayo inaendelea kufanyika.

Amesema moja ya masuala yaliyokuwa yakitiliwa mkazo katika mkutano uliohusu biashara ya kuuziana umeme na kununua umeme kwa nchi Wanachama Mashariki mwa Afrika (EAPP) ni uunganishaji umeme kati ya Tanzania na Kenya.

“Na leo laini hii ya umeme ya kV 400 imewashwa imezinduliwa rasmi, nimpongeze Dk Biteko na Rais Samia kwa jitihada hizi kubwa,” amesema Kapinga.

Katibu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema sasa nchi inazalisha zaidi ya megawati 3000 za umeme hali inayoifanya Tanzania kuwa nchi inayozalisha umeme mwingi kuliko nchi zote za Afrika Mashariki.

“Hali hii inatoa fursa kwa Tanzania kufanya biashara ya umeme na nchi nyingine za Afrika ikiwamo Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya,” amesema Mramba.

Amesema mradi huo utaenda katika kanda mbalimbali ikiwemo mikoa ya Kaskazini na kuingia hadi nchini Kenya.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga amesema mradi wa kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma umegawanyika katika sehemu kuu mbili,  ambazo ni  ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme katika msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 345 na upanuzi wa vituo vya kupokea na kupoza umeme vya Chalinze (400/220/132kV) mkoani Pwani na Zuzu (400/220/33kV) mkoani Dodoma.

Amesema malengo ya mradi huo ni kuwezesha usafirishaji wa umeme wote (2,115MW) utakaozalishwa katika Bwawa la JNHPP na kuufikisha kwenye maeneo yote ya mahitaji ya umeme.

Amesema lengo lingine kuwezesha kazi ya uunganishaji umeme kwa pamoja katika mifumo ya Mashariki mwa Afrika (Eastern Africa Power Pool – EAPP) na Kusini mwa Afrika (Southern Africa Power Pool – SAPP) na hivyo kuwezesha kufanyika kwa biashara ya nishati ya umeme kikanda.

Ameongeza kuwa, mradi husika unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 ukigharimu Sh513 bilioni na mkandarasi  Kampuni ya TBEA kutoka China ambayo imeshalipwa malipo ya awali ya Sh107.93bilioni sawa na asilimia 20 ya gharama za mradi.

Related Posts