“Tumefanikiwa kuwarudisha tembo 61 Hifadhini” Waziri Kairuki

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imedhamiria kutatua changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori huku ikisisitiza kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 imeweka kipaumbele katika kutatua changamoto hiyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) wakati wa zoezi la kuwarudisha tembo hifadhini lililofanyika Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya leo Mei 9,2024.

“Tumefanikiwa kuwarudisha hifadhini tembo takriban 61 na leo tumefukuza tembo 18” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Amesema hiyo inathibitisha umakini wa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujali usalama wa maisha ya wananchi na mali zao na uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori na misitu.

Waziri Kairuki amesisitiza kuwa Serikali itafanya kila liwezekanalo kutatua changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu nchini hususan tembo, Simba fisi madoa, chui, mamba, kiboko, nyani na tumbili.

“Tutaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa kila aina ya wanyama na mikakati ya wanyama husika” amesisitiza.

Amesema zoezi hilo la kufukuza tembo kwa kutumia helikopta limeambatana na kufunga mikanda ya mawasiliano kwa tembo viongozi wa makundi mbalimbali ambapo mpaka sasa imeshafungwa mikanda miwili lakini zoezi litamalizia kwa mkanda wa tatu.

Pia, amesema Rais Samia ameelekeza kwamba wananchi walioathirika na wanyamapori wakali na waharibifu walipwe kifuta jasho/machozi
katika vijiji vya Igunda , Rujewa, Mapogoro, Mlungu, lwalanje,Vikaye, Nyeregete, Manyenga na Mwanavala.

Aidha, Mhe. Kairuki amezielekeza Taasisi za TANAPA, TAWA na TFS kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi mazingira na namna ya kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu pindi wanapovamia makazi yao.

Mkutano huo umehudhuriwa na Watendaji, Maafisa Waandamizi na Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii,TAWA, TAWIRI, TANAPA, TFS, viongozi wa Chama pamoja na wananchi.

Related Posts