Uchunguzi bado kesi ya jengo lililoporomoka Kariakoo

Dar es Salaam. Upande wa Jamhuri umesema upelelezi unaendelea katika kesi ya kuua bila kukusudia inayowakabili wanaodaiwa kuwa wamiliki wa jengo lililoporomoka Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo.

Mshtakiwa Awadh Ashour( aliyejifunika uso kushoto) anayekabiliwa na mashtaka ya 31 ya kuua bila kukusudia, akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi hiyo kuahirishwa. Picha na Hadija Jumanne

Wamiliki hao, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ni Leondela Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam (61) wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour (38) wa Ilala.

Mshtakiwa Zenabu Islam (mwenye baibui) anayekabiliwa na mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia, akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi hiyo kuahirishwa. Picha na Hadija Jumanne

Mdete na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia katika kesi ya mauaji namba 33633/2024 iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mshtakiwa Leondela Mdete ( mwenye dera jekundu), anayekabiliwa na mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia, akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi hiyo kuahirishwa. Picha na Hadija Jumanne

Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele leo Alhamisi Desemba 12, 2024 ameieleza mahakama kwamba upelelezi haujakamilika kesi ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Mwakamele ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Geofrey Mhini.

“Mheshimiwa hakimu, washtakiwa wote wapo ndani ya mahakama na kesi yao imeitwa leo kwa ajili ya kutajwa, upelelezi bado unaendelea, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amesema.

Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hadi Januari 13, 2025 itakapotajwa. Washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Washtakiwa walitimiza masharti matatu ya dhamana yaliyotolewa na Hakimu Mhini ambayo yalimtaka kila mshtakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka serikali za mitaa.

Pili, wadhamini walitakiwa kusaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja na tatu, wadhamini walitakiwa wawe wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa walifikishwa mahakamani Novemba 29, 2024 na kusomewa kesi ya kuua bila kukusudia.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume cha kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Novemba 16, 2024 katika mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha kifo cha Said Juma.

Katika shtaka la pili hadi la 31, washtakiwa wanadaiwa  siku na eneo hilo walisababisha kifo cha Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu na Catherine Mbilinyi.

Wengine ni Elton Ndyamukama, Mariam Kapekekepe, Elizabeth Kapekele, Hadija Simba, Frank Maziku, Rashid Yusuph, Ally Ally, Ajuae Lyambiro, Mary Lema na Khatolo Juma.

Pia, wanadaiwa isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusabisha kifo cha Sabas Swai, Pascal Ndunguru, Brighette Mbembela, Ashery Sanga, Venance Aman, Linus Hasara, Pascalia Kadiri, Issa Issa, Lulu Sanga, Happyness Malya na Brown Kadovera.

Related Posts