MSIMU huu wa 2023/24, hakuna mbabe kati ya Ihefu SC na JKT Tanzania baada ya timu hizo kushindwa kufungana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida huku suluhu hiyo ikiziachia maswali ya kwamba itakuwaje mechi nne zilizosalia?
Leo timu hizo zilikutana kwa mara ya pili msimu huu ndani ya Ligi Kuu Bara ambapo Ihefu walikuwa wenyeji. Kumbuka ule mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam wakati JKT Tanzania wakiwa wenyeji matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.
Katika mchezo wa leo ambao ulitawaliwa na matumizi makubwa ya nguvu, Ihefu ilikuwa ikipambana kupata ushindi ili kupanda hadi nafasi ya saba kutoka ya 11 na kuishusha JKT Tanzania.
Lakini pia JKT Tanzania nayo ilikuwa ikiusaka ushindi kama huo ili kulikimbia zaidi eneo hatari la kushuka daraja na kufikisha pointi 32 ambazo zingewaweka nafasi ya saba kwa kujiamini. Hesabu zao zote zimekwama ingawa kila upande umepiga hatua moja mbele.
Suluhu hiyo imeifanya Ihefu kupanda nafasi moja kutoka 11 hadi 10 baada ya kufikisha pointi 29 sawa na Singida Fountain Gate, huku JKT Tanzania nayo ikipanda nafasi moja kwa kufikisha pointi 30 sawa na Kagera Sugar.
JKT Tanzania yenyewe imekaa nafasi ya saba na kuishusha Kagera Sugar kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Zote zikicheza mechi 26 na kukusanya pointi 30.
Ihefu na JKT Tanzania zimekuwa na ushindani mkubwa kila zinapokutana ambapo katika mara nne walizokutana ndani ya Ligi Kuu, JKT Tanzania imeshinda mechi moja huku sare zikiwa tatu. Msimu wa 2021/22, timu hizi zilikuwa katika Ligi ya Championship ambapo Ihefu iliibuka kidedea ugenini na nyumbani ambapo kote ilishinda kwa mabao 2-0.
Sare ya leo bado imeziweka timu hizo kwenye wasiwasi wa kusalia ndani ya ligi kwani katika mechi nne zilizosalia timu iliyopo nafasi ya mwisho inaweza kukaa juu yao kimahesabu.
Ipo hivi, Mtibwa Sugar iliyopo mkiani na pointi 20, katika mechi nne zilizosalia zenye pointi 14 ikishinda zote itafikisha 34 ambazo hivi sasa inazo Coastal Union inayoshika nafasi ya nne, hivyo kimahesabu bado JKT Tanzania na Ihefu hazipo salama lazima zikaze buti dakika za mwisho.
Ihefu ina nafasi ya kujiuliza katika mechi nne zilizosalia dhidi ya Tanzania Prisons (ugenini), Tabora United (ugenini), Dodoma Jiji (nyumbani) na Mtibwa Sugar (nyumbani).
JKT Tanzania iliyopanda daraja msimu huu, nayo katika mechi nne zilizosalia itatakiwa kuzichanga vyema karata zao itakapocheza dhidi ya Singida Fountain Gate (nyumbani), Azam (nyumbani), Coastal Union (ugenini) na Simba (ugenini).