Dodoma. Changamoto ya ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa linaloweza kumudu kupita barabara mbaya limepatiwa ufumbuzi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Hospitali hiyo imepata gari aina ya Toyota Land Cruiser (Hardtop) lenye kitanda cha mgonjwa, mtungi wa oksijeni na mkoba wa dawa.
Gari hilo limekabidhiwa leo Alhamisi Mei 9, 2024 na Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde.
Akikabidhi gari hilo, Mavunde amesema Februari 2, 2024 alikabidhi magari mawili ya wagonjwa kwa hospitali hiyo ambayo hayawezi kwenda katika barabara zenye hali mbaya (changarawe na udongo).
Amesema hospitali iliomba kupatiwa gari ambalo linaweza kufika katika mazingira tofauti na yale yenye barabara bora za lami.
Mavunde ambaye pia ni Waziri wa Madini, amesema kutokana na ombi hilo, aliahidi kwenda kuzungumza na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuhusu upatikanaji wa gari la kubebea wagonjwa la uhakika kwenye hospitali hiyo.
Amesema waziri kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan alipokea maombi na leo amekabidhi gari la tatu la wagonjwa katika hospitali hiyo, ili kuboresha huduma.
Mavunde amesema hatua hiyo itawafanya Watanzania wengi kupata huduma za afya kwa haraka na katika mazingira yoyote, kwa sababu gari hilo lina uwezo wa kusafiri umbali mrefu na kwa kasi kubwa tofauti na ya awali.
Amesema hospitali hiyo haihudumii watu wa Dodoma pekee, hivyo wanao wajibu wa kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendelea kuboreshwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Alphonce Chandika amesema gari hilo lina uwezo wa kwenda masafa marefu zaidi na kutumika kwenye barabara zisizo nzuri.
“Lina uwezo wa kumfuata mgonjwa sehemu yoyote ile hata kama ikiwa ni kijijini ambako barabara si nzuri,” amesema.
Amesema baada ya kupatiwa magari ya awali, walibaini wanaweza kuhitajika kumfuata mgonjwa kutoka kwenye zahanati au hospitali za wilaya, hivyo waliwasiliana na Mavunde aliyeahidi kwenda kuzungumza na mamlaka husika waweze kupata gari linalomudu huduma hiyo.
Dk Chandika amesema kupatikana kwa gari hilo, kutawawezesha kuwafuata wagonjwa popote walipo bila kujali hali ya barabara watakayopita.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Kaspar Muya amesema gari hilo ni miongoni mwa mapambano ya kuondoa vifo vya wajawazito, watoto, na visivyo vya lazima vinavyotokana na kuchelewa kupata huduma kutokana na umbali na kukosekana usafiri.
Hospitali ya Benjamin Mkapa inahudumia wagonjwa 1,000 kila siku, tangu ilivyoanza kutoa huduma Oktoba 13 mwaka 2015.