Mwanza. Hujafa hujaumbika, ndivyo anavyoanza kusimulia mzee Mukama Vedastus, aliyekatwa mkono wa kulia baada ya kuliwa na mamba wakati akivua samaki.
Anasema bila ujasiri wa kukandamiza vidole vyake machoni mwa mamba, maisha yake yangebaki kuwa historia, kwani mnyama huyo alidhamiria kumuua.
“Nikikumbuka huwa naamini nguvu ya Mungu, kwani (mamba) alishanitoa utumbo nje, ingawa hakuwa ameutoboa, waliokuja kuniokoa waliuingiza ndani,” anasema mzee Vedastus, mkazi wa Kijiji cha Buhama, kitongoji cha Igoma katika Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.
Anaongeza: “Nilipofika hospitali wakati wananishona hapa tumboni (huku akionyesha jeraha) walianza kuchambua mavitu, ikiwamo matakataka kuyatoa kwenye nyama za tumboni ili wanishone. Yule mamba ilikuwa aniue.”
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu yaliyofanyika nyumbani kwake kijijini hapo, Mukama anasema ilikuwa saa tisa alasiri akiwa anaendelea na shughuli za uvuvi kwenye Ziwa Victoria na alishtukia mkono wake ukiwa umeshikiliwa na mamba.
“Nilipambana na mamba kama unavyoona mbwa wakipigana jinsi anavyosimama, huku mkono wangu wa kulia akiwa ameung’ang’ania ila alikuwa ananizidi nguvu kwa kuniangusha kwenye maji mara kwa mara na nikijitahidi kuinuka, naye akiwa bado kaung’ata mkono wangu akiendelea kunijeruhi maeneo ya tumboni.
“Nilikuwa ninapata maumivu makali, lakini nilijiambia ukikata tamaa umekwisha, hivyo nikaendelea kupambana, nikiwa nimeanza kuchoka na maumivu kuwa makali na damu nyingi kuvuja nikapata wazo kuwa watu wanasemaga ukimziba macho mamba anakuachia.
“Kwa kutumia mkono wa kushoto nilikandamiza vidole vyangu viwili cha shahada na gumba machoni kwa mamba kwa nguvu zangu zote, huku nikiwa nimefumba macho nikisema liwalo na liwe, kwa mshangao mamba aliniachia na kuangukia kwenye maji,” anasema na kuongeza:
“Nami nikakimbilia nchi kavu kwa kujivuta, huku nikipiga kelele, wananchi walikuja na kuniwahisha hospitali.”
Mukama anafafanua kuwa alikuwa akivua katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 20, hakukuwa na mamba wengi kama waliopo wakati huu.
“Siku hizi siendi kuvua tangu nilipopata ajali hii, ila kila mara nasikia watu wanaliwa na mamba, wakiwamo watoto wa ndugu zangu. Hali ni mbaya.
“Wanakamata na kuwala mpaka bata wakiwa wanazunguka zunguka mwaloni. Naishauri Serikali ingewavuna, kwani kwa namna nilivyoumia nikiwakamata nitawaua sheria itakuja baadaye,” anasema mzee Mukama.
Anasema: “Kibaya zaidi hata ukifuatilia hiyo pole mlolongo ni mrefu sana, nikiwa nimelazwa ndugu yangu alikuwa anafuatilia, lakini alishindwa baada ya kusomewa vifungu vya sheria ambavyo sivikumbuki, ninachojua alichoambiwa ni kuwa mimi ndiye niliyemfuata mamba ziwani.”
Anasema ana watoto wanane wanaomtegemea na kazi aliyokuwa akifanya ni uvuvi pekee, hivyo tangu apate ajali hiyo havui tena, hali ya kimaisha imekuwa ngumu.
“Angalia mwenyewe siwezi kufanya kitu chochote kwa sasa, haya ndiyo maisha yangu, watoto hawana mavazi, chakula ni shida na niliambiwa nimemfuata mamba ziwani, hivyo sijapewa hata senti tano,” anasema mzee Mukama.
Mwathirika mwingine, Maina Stephano, anasimulia tukio la kushambuliwa na mamba mwaka 2018 alipokwenda kutega nyavu kwa ajili ya kuvua samaki.
“Nilipomaliza kutega nataka kutoka kwenye maji naogelea kurudi mwaloni, alinikamata. Sikujua nimekamatwa na nini, nikajua ni kitu tu cha majini nitoke nikaangalia nje ya maji, ile najaribu kujitikisha, tulizungushana sana, alitaka kunirudisha ziwani,” anasema.
Stephano anaeleza kuwa walisumbuana sana na mamba kabla ya kuzidiwa nguvu. “Akanirudisha majini, akawa ameinua mguu wangu juu, nauona unaelea kwenye maji akiwa ameng’ata eneo kati ya nyonga na makalio. Nikapata ujasiri na kuingiza vidole vyangu wote viwili kwenye macho yake. Hapo akaniachia na kurudi kwenye maji,” anasema.
Stephano anasema alijikuta na majeraha matatu nyuma kwenye makalio, kwani mnyama huyo aliondoka na nyama ya kwenye paja na jeraha lingine mgongoni ambalo lilikuwa na maumivu zaidi. “Nilitibiwa kwa miaka mitatu, nilichoma sindano nne za tetenasi na nikatumia dawa. Nilikaa nyumbani kwa miezi mitatu kabla ya kuanza tena shughuli za uvuvi,” anasema. Mpaka sasa Stephano bado anahisi maumivu. “Eneo la paja na kalio mpaka sasa huwa ninasikia ganzi, kuna wakati mguu unagoma hata kutembea.” Katika matukio mengine, anasema kuna vijana kadhaa walikamatwa na mamba, mwingine alishikwa mguu ukatobolewa, lakini hakufa.
Komanya Kayungilo ni miongoni mwa vijana waliopata madhila ya kuliwa na mamba na kunusrika kifo. Anasema walikuwa wanakwenda kuvua katika kijiji cha Izindabo, kata ya Buhama kisiwani Kome Mchangani, wakiwa wanane na mitumbwi miwili na kila mmoja ulikuwa na watu wanne.
Anasema hajui nini kilitokea, lakini alijikuta akivutwa mguu na mamba na kutahamaki wenzake wote walikuwa wamemkimbia, hivyo akabaki ametulia kama aliyekufa kwa dakika 15 akiwaza afanye nini kujinasua, akiamini akijitikisa atamalizwa.
“Taratibu nikajigeuza na kuangalia macho yake yalipo, kisha kwa kasi sana nikakandamiza vidole viwili machoni mwake akapoteza mwelekeo na kuniachia, nikajivuta kwenda kwenye mtumbwi kando ya maji, ghafla tena mamba akawa anarudi kwa kasi kuja kunivaa, bahati ilikuwa yangu, pembeni kulikuwa na kijana aliyempiga na fimbo kwa nguvu likakimbilia majini.
“Yule kijana akaita watu wakaja kunichukua na kunipeleka hospitalini kwa ajili ya matibabu na nilishonwa jeraha la mguuni.
“Kama unavyouona mguu umekuwa mdogo na hauna mawasiliano, kati ya kiwiko kwenda chini, sihisi chochote, kumekufa ganzi, nilijiuguza kidonda wiki mbili nikarudi kazini kwa sababu nina familia ya watoto 12, isingekuwa rahisi kukaa tu,” anasema Kayungilo.
Kayungilo anasema hata alipokuwa akijitibu alikuwa akipewa pesa za pole na wenzake, anatuma kijijini Busisi ambako familia yake inaishi.
“Naomba wahusika waendelee kutoa elimu kuhusu suala hili, kwani tulio wengi hatuna elimu ya kuchukua hatua ikiwamo kupata hiyo fomu sijui hati ya matibabu ili Serikali itulipe huo mkono wa pole,” anasema Kayungilo.
Itaendelea kesho kuona hatua zinazochukuliwa kupunguza na kuondoa athari.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.