Mamilioni ya raia wa Umoja wa Ulaya wanaotarajiwa kupiga kura kati ya Juni 6 – 9, kuwachagua wajumbe 720 wa Bunge la umoja huo wanaghadhabishwa na hali ngumu ya maisha, inayowakabili kila kukicha.
Hali inayoweza kuathiri vyama vikuu kwenye uchaguzi wa chombo hicho muhimu katika kutunga sera za masuala mbalimbali ikiwemo biashara katika umoja huo wenye nchi 27.
Tangu uchaguzi uliopita mwaka 2019, Uchumi wa Ulaya umepata mapigo ikiwemo kufungwa kwa biashara wakati wa janga la COVID-19, kupanda kwa bei ya bidhaa kote ulimwenguni na hata kuathiriwa zaidi na bei ya juu ya nishati iliyochochewa na uvamizi wa Urusi ndani ya Ukraine.
Usaidizi mkubwa wa serikali kwa familia na biashara uliisaidia kuepusha mdororo mkubwa wa Uchumi. Lakini kama tu ilivyo Marekani ambapo juhudi hizo hazionekani kumsaidia sana Rais Joe Biden kwenye kampeni zake kuwania muhula mwingine wa urais Marekani, huenda usiwe chachu ya kutosha kwa viongozi wa Ulaya kuutumia kushawishi uungwaji mkono.
Ustahimilivu dhidi ya mapigo ya kiuchumi
Jeromin Zettelmeyer, mkurugenzi wa taasisi ya kiuchumi Bruegel iliyoko Brussels Ubelgiji, amesema inashangaza jinsi Ulaya imeweza kustahimili mapigo hayo, lakini ustahimilivu huo si jambo linaloleta matumaini makubwa.
Ameongeza kuwa wakati mwingine unahitaji kuanza kufikiria raia wa nchi yako kwanza, kabla ya wengine.
Kwa mfano rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anapaswa kuyapa kipaumbele masuala ya Wafaransa kama nyumba za bei nafuu, badala ya kufuatilia msaada kwa Ukraine katika vita vyake dhidi ya Urusi.
Kitisho cha ongezeko la Umaskini
Kwa sasa, vyama vikuu, ambavyo vina ushawishi mkubwa katika Bunge la Ulaya na vilevile katika siasa za ndani ya nchi zao, vina karibu mitazamo inayofanana ya kuwa na biashara ya wazi na mataifa mengine ulimwenguni.
Chama cha Le Pen chazindua kampeni uchaguzi wa Bunge la Ulaya
Lakini makubaliano hayo yako hatarini kwani raia wengi wa Ulaya wanaungana kwa kauli moja kwamba hali ya uchumi iliyopo haifanyi kazi kwao.
Mwaka uliopita pato la Ulaya likikua kwa asilimia 0.5, huku ukosefu ajira ukiwa asilimia 6.5 hiyo ikiwa chini kuwahi shuhudiwa katika historia yake.
Lakini tathmini ya ndani ya takwimu hizo zinakuacha na mshangao wa jinsi mamilioni ya raia wa Ulaya wakiwemo wanaofanya kazi wanatatizika na upungufu wa fedha kuyakidhi mahitaji yao.
Kulingana na utafiti wa kila mwaka wa taasisi ya R+V ya Ujerumani, masuala matatu makubwa kwa Wajerumani yamefungamana na fedha, ikiwemo gharama ya juu ya maisha, kodi ya juu ya nyumba na hofu ya kupunguzwa kwa ruzuku au michango ya serikali.
Hofu ya raia kutoweza kuyakidhi mahitaji yao
Isabelle Borucki, profesa katika chuo kikuu cha Philipps Maarbug Ujerumani amesema, raia wanahofu ikiwa wataweza kuyakidhi mahitaji yao kifedha.
Hofu kama hiyo pia inashuhudiwa Uhispania, Poland na kwingineko ambako viwango vya riba kwa wamiliki majumba vimeongezeka.
AfD kuamua wagombea wake katika bunge la Ulaya
Jinsi masuala hayo yote yatakavyoathiri bunge la nchi 27 wanachama, hakika itategemea masuala mengine ikiwemo siasa na miungano itakayoundwa kuelekea uchaguzi huo.
Kura za maoni zinaonesha vyama vikubwa vya mirengo ya kulia na shoto vikiongoza katika nchi 16. Lakini pia zinaonesha makundi yenye misimamo mikali yakijiongezea ushawishi kuwa na uwezo wa kushinda moja juu ya tano ya viti vya bunge la Ulaya. Na hali ya watu kutoridhishwa na hatua za kiuchumi huenda inachangia hayo.
(Chanzo: RTRE)