Yanga yaitingisha Mazembe, mabeki wawili wakitajwa

MSAFARA wa kikosi cha Yanga wenye wachezaji 25 kimeondoka mchana wa leo kwenda Lubumbshi, DR Congo, tayari kwa ajili ya mechi ya tatu ya Kundi A ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi TP Mazembe, huku benchi la ufundi la wenyeji likitoa kauli kuonyesha namna gani ina kazi kubwa kukabiliana na Wananchi.

Yanga imeondoka na mastaa karibu wote isipokuwa Jean Baleke anayecheza kwa mkopo Jangwani akitokea Mazembe na itashuka uwanjani keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Mazembe kukabiliana na  wenyeji wao ambao misimu miwili iliyopita iliwafumua nje ndani katika mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho.

Kikosi hicho kikiongozwa na kocha Sead Ramovic, kinaenda kukabiliana na Mazembe huku ikitoka kupoteza mechi mbili mfululizo za awali mbele ya Al Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria, kitu kilichomtisha kocha aliyekuwapo wakati Vijana w Jangwani wakisambaratisha Mazembe nje ndani.

Mechi hiyo ni muhimu kwa timu zote, lakini kumbukumbu ya mara mwisho zilipokutana kwenye uwanja huo na matokeo iliyopata kwa kila mmoja yamempa presha zaidi kocha msaidizi Pamphil Mihayo.

Mara ya mwisho Yanga kucheza uwanja huo ilishinda kwa bao 1-0 baada ya awali kuifunga mabao 3-1 Kwa Mkapa katika mechi za makundi za Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023 ambapo vijana wa Jangwani walifika hadi fainali na kulikosa taji mbele ya USM Alger ya Algeria kwa kanuni za faida ya bao la ugenini.

Katika mchezo wa kwanza wa fainali hizo, Yanga ilifungwa 2-1 kisha kwenda kushinda ugenini jijini Algers kwa bao 1-0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2 na Waalgeria wakalibeba taji hili kiulaini licha ya kutibuliwa nyumbani na wababe hao wa soka la Tanzania.

Licha ya Mazembe kubadilisha kikosi hadi kocha wakimrudisha Lamine Nd’iaye aliyewarudishia ubora, lakini kocha msaidizi wa Msenegali huyo, Pamphil Mihayo ameliambia Mwanaspoti anajua kabisa mchezo dhidi ya Yanga hautakuwa rahisi.

Kiungo huyo wa zamani wa Mazembe, anayemsaidia Nd’iaye aliliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka DR Congo, alisema Yanga ni timu isiyotabirika na kupoteza kwao michezo miwili iliyopita ya kundi hilo, ndio kitu kitakachoongeza ugumu katika mechiyo ya kesho.

Kocha huyo aliongeza, ni bahati mbaya kwa Mazembe ni kukutana na Yanga, huku ikiwa  imetoka kupoteza mbele ya Al Hilal kwa mabao 2-1 ikiwa ugenini baada ya awali kupata suluhu na MC Alger, hivyo itakuwa ina presha kubwa zaidi kukabiliana na wageni hao walipoteza mara mbili mbele ya Al Hilal na MC Alger.

Hata hivyo, alisema kwa kutambua ugumu wa pambano hilo benchi la ufundi limekuwa likipambana kurudisha morali kwa wachezaji kwa kuwasaidia kisaikolojia kabla ya mchezo huo.

“Hii mechi ni ngumu sana (dhidi ya Yanga), wana wachezaji waliokomaa vizuri ukiona rekodi yao Afrika imebadilika sana, wamepoteza mechi mbili zilizopita, hivyo mchezo huu utakuwa kama ni fainali kwao na hii ndio hofu yetu,” alisema Mihayo na kuongeza;

“Tutalazimika kuwa makini sana kwenye mechi hii, unaona na sisi (Mazembe) tunatoka kupoteza mechi iliyopita, saikolojia ya wachezaji tutahitaji kuiweka sawa kabla ya mechi inayofuata.”

Aidha Mihayo alisema wanataka kuusaka ushindi katika mechi hiyo ili kujiweka sehemu salama kabla ya timu hizo kurudiana wiki ijayo.

“Unajua baada ya mchezo huu tutarudiana kwa kuja hapo Tanzania, tunataka kushinda hii mechi ili tuweke hesabu zetu sawa ingawa haitakuwa rahisi kabisa, alisema Mihayo.

Yanga ilifanya mazoezi ya mwisho juzi kwenye Uwanja wa KMC wenye nyasi bandia ikiwa ni mbinu maalum kwa wachezaji ili kujiandaa na kuutumia vyema Uwanja wa Mazembe ambao una nyasi kama hizo na jana ilipaa kuwahi mchezo huo, huku wachezaji na benchi la ufundi wakiahidi mambo mazuri kwa mashabiki.

Hili litakuwa pambano la tano kwa Yanga na Mazembe kukutana katika michuano ya CAF kwa miaka ya karibuni, baada ya awali pia kupangwa kundi moja katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho 2016 ambapo Wakongo walishinda nje ndani kabla ya kugeuziwa kibao zilipokutana tena Shirikisho 2022-2023.

NYOTA wa TP Mazembe Mnigeria Suleman Shaibu amesema licha ya mwenendo wa Yanga msimu huu ila ina kikosi chenye wachezaji bora wanaoweza kuwapa matokeo chanya, huku akiwataja beki wa kati, Dickson Job na kiungo mshambuliaji, Stephane Aziz Ki.

Mchezaji huyo amezungumza hayo wakati timu hizo zikitarajia kupambana kesho katika mchezo wa tatu wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kwenye Uwanja wa Tp Mazembe, huku miamba hiyo kwa pamoja ikihitaji pointi tatu.

“Yanga ni timu ambayo huwezi kuidharau kwa sababu ya mwenendo mbovu wa matokeo yao ya hivi karibuni, nawaheshimu sana Dickson Job na Aziz Ki kutokana na mchango wao tangu nimeanza kuwaona wakicheza, kuanzia msimu huu na hata uliopita.”

Suleman ambaye kwa sasa anacheza nafasi ya ushambuliaji tofauti na awali alivyokuwa anacheza nafasi ya kipa, alisema Job alimuona tangu walivyokutana nao Kombe la Shirikisho na ndipo akamvulia kofia kutokana na jinsi alivyokuwa anacheza.

“Jamaa anajua sana kusoma hatari za wapinzani na hata ukiangalia mchezo ule ulivyokuwa alituzuia ipasavyo, Aziz Ki ni kweli uwezo umeshuka tofauti na msimu uliopita lakini ni mchezaji pia ambaye namuheshimu na anajua kufunga,” alisema.

Katika Ligi ya DR Congo ‘Linafoot’ ambayo huchezwa kwa mfumo wa makundi, Shaibu amefunga mabao matatu katika michezo mitano kati ya minane ya timu hiyo ilichocheza, huku akichaguliwa pia mchezaji bora wa mchezo mara moja kwa msimu huu.

Timu hizo zinakutana zikiwa na matokeo yanayofanana katika michezo yao iliyopita ambapo Yanga ilichapwa mabao 2-0, dhidi ya MC Algers ya Algeria ikiwa ni kichapo cha pili mfululizo baada ya kuchapwa pia mechi ya kwanza 2-0 na Al Hilal kutoka Sudan.

Kwa upande wa TP Mazembe inaingia katika mchezo huo wa kundi ‘A’ ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 2-1, mechi yake iliyopita na Al Hilal, huku ikiambulia pointi moja tu baada ya kulazimishwa suluhu na MC Alger ya Algeria nyumbani.

Katika kundi hilo la ‘A’ Al Hilal inaongoza ikiwa na pointi zake sita, ikifuatiwa na MC Alger yenye nne nafasi ya pili huku TP Mazembe ikishika ya tatu na pointi moja, wakati Yanga iko mkiani bila ya pointi baada ya kuchapwa mechi mbili.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana ilikuwa ni Kombe la Shirikisho Barani Afrika hatua ya makundi ambapo zilipangwa kundi ‘D’ na Yanga ilishinda kwa bao 1-0, lililofungwa na Farid Mussa, mechi iliyopigwa DR Congo Aprili 2, mwaka jana.

Kichapo hicho kilikuwa cha pili kwa Mazembe katika kundi hilo msimu huo baada ya mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam, Yanga kushinda 3-1, Februari 19, 2023, yaliyofungwa na Kennedy Musonda, Mudathir Yahya na Tuisila Kisinda ‘TK Master’.

Bao pekee la kufutia machozi kwa upande wa Mazembe katika mchezo huo lilifungwa na aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Alex Ngonga.

TP Mazembe ilifuzu hatua ya makundi baada ya kuanzia raundi ya pili kwa kuitoa Red Arrows ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-1, baada ya mchezo wa kwanza kushinda ugenini mabao 2-0, kisha mechi ya marudiano DR Congo kuibuka kidedea na ushindi wa 2-1.

Yanga ilifika makundi ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo kwa rekodi ya aina yake baada ya kufuzu kwa jumla ya mabao 17, kwani katika mechi zake za raundi ya awali iliweza kuiondosha Vital’O kutoka Burundi kwa jumla ya mabao 10-0.

Baada ya Yanga kufuzu hatua ya hiyo ya awali, ikakutana na CBE SA ya Ethiopia ambapo mechi yake ya kwanza ikiwa ugenini ilishinda bao 1-0, huku mchezo wa marudiano uliopigwa Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar ikashinda mabao 6-0.

Related Posts