Na WILLIUM PAUL, ROMBO.
RAIS Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuongoza maelfu ya wananchi katika mashindano ya riadha yajulikanayo kama Rombo marathon and Ndafu Festival Disemba 23 mwaka huu wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza leo na waandishi wa habari kuelekea mashindano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mangwala alisema kuwa, maandalizi yote yanaenda vizuri ambapo wa natarajia kuwa na wakimbiaji 3000 watakaokimbia kilomita 21, 10 na 5.
Alisema kuwa, mbio hizo ambapo kwa mwaka huu ni msimu wa tatu ni mbio na kukimbilia msituni ambapo itatoa fursa kwa washiriki kujionea vivutio mbalimbali vya utalii pamoja na vyakula vya asili vya kabila la wachaga.
“Watakaokuja katika mbio za Rombo marathon hawatajutia kwani watashuhudia mambo mengi ya asili lakini pia ni fursa ya kupumzisha akili na kuwaza mwaka mzima umefanya nini na unaenda kuanza vipi mwaka mpya kwa nguvu na hari kubwa” Alisema Mangwala.
Aidha alisema kuwa, walijipanga kuhakikisha swala la ulinzi linaimarishwa ili washiriki wote wanakuwa salama wanapoingia na kutoka katika wilaya hiyo ya Rombo na kuwasihi wananchi kuendelea kujiandisha kushiriki mbio hizo.
Mkuu huyo wa wilaya alidai kuwa, fedha zitazopatikana kupitia mbio hizo zitatumika katika kujenga matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari wilayani Rombo pamoja na kuchangia katika ujenzi wa hospitali ya Huruma ili kuwa hospitali ya rufaa yenye hadhi ya mkoa ili wananchi wa Rombo wapate huduma muhimu na bora katika hospitali hiyo.