Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Kampuni ya Asas imeonyesha dhamira yake ya kuendeleza sekta ya ufugaji na kuboresha maisha ya jamii kwa kutekeleza ahadi iliyotolewa wakati wa Sherehe za Kizimkazi Festival kwa kuandaa ziara ya mafunzo kwa wafugaji kutoka Kizimkazi hadi mashamba yake ya kisasa yaliyopo mkoani Iringa.
Ahadi hiyo, iliyotolewa Agosti 8, mwaka huu, imelenga kuwapa wafugaji wa Kizimkazi maarifa ya kisasa katika ufugaji wa mifugo. Ziara hiyo imefanikiwa kuwafikia wafugaji wapatao 50 ambao walipata nafasi ya kujifunza mbinu bora za malisho, matibabu ya mifugo, na usindikaji wa maziwa, huku wakielezwa jinsi ya kuboresha uzalishaji na kudumisha afya ya mifugo yao kwa njia endelevu.
“Ziara hii imefungua macho yetu na kutupa maarifa mapya. Ikiwa maarifa haya yatatumika vizuri, hakika yatasadia kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha ya wafugaji wa Kizimkazi,” alisema msemaji wa kampuni ya Asas, akibainisha kuwa ahadi hii imetekelezwa kwa mafanikio makubwa.
Kwa miaka mingi, Asas imejidhatiti kuunga mkono maendeleo ya sekta ya kilimo na ufugaji, ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji wake wa kijamii. Msemaji wa kampuni hiyo aliongeza: “Utekelezaji wa ahadi hii unadhihirisha dhamira yetu ya kusaidia wafugaji wadogo kuongeza kipato na kuboresha ustawi wa jamii zao.”
Ziara hiyo, ambayo inachukuliwa kama mwanzo wa ushirikiano wa kudumu, inatarajiwa kuleta mabadiliko chanya kwa wafugaji wa Kizimkazi na maeneo mengine nchini. Asas imeweka wazi kuwa itaendelea kushirikiana na wafugaji ili kuimarisha sekta ya ufugaji kupitia uwekezaji wa vitendo katika elimu na mafunzo.
Kwa utekelezaji huu, kampuni ya Asas imethibitisha kuwa sekta binafsi inaweza kuwa mshirika muhimu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kusaidia kuimarisha maisha ya jamii za wafugaji nchini Tanzania.