MIEZI michache baada ya aliyekuwa mfadhili na Rais wa Biashara United, Revocatus Rugumira kujiweka kando na kuirejesha timu hiyo kwa wananchi mambo yameanza kuwa magumu ikishindwa kujiendesha na kusababisha baadhi ya wachezaji kuondoka.
Mwanaspoti lilidokezwa mapema kwamba wachezaji walitimka ndani ya klabu hiyo kwa sasa ni; Ditram Nchimbi, Sadalla Lipangile, Fredson Elisha na Faustine Kulwa ambaye juzi amerejea baada ya kupigiwa simu na uongozi kwa ahadi kuwa mambo yatakuwa sawa.
Timu hiyo ambayo msimu uliopita ilifanya vizuri na kucheza mtoano kusaka nafasi ya kupanda Ligi Kuu, msimu huu kutokana na ukata imeshinda mechi mbili kati ya 10, ikipata sare nne na kupoteza nne na kuvuna alama 10 ikikamata nafasi ya 11.
Akizungumzia hali hiyo, mshambuliaji Ditram Nchimbi aliliambia Mwanaspoti, wachezaji hawajalipwa mishahara yao kwa muda wa miezi mitatu, hivyo, amerudi nyumbani kusubiria hali ikae sawa ama atafute malisho mahali pengine kwenye usajili wa dirisha dogo.
“Ni kweli siko na timu kwa sasa maana nje ya uchumi wa timu kuyumba ila nilikuwa na dharura nyumbani kwahiyo niko nyumbani maana si umesikia kuwa timu imeshindwa hata kusafiri hatujalipwa mishahara miezi mitatu wala signing fee (fedha za usajili),” alisema Nchimbi na kuongeza;
“Hivyo kama tunapambania kesho zetu tu, ila kimaslahi timu hali ni mbaya sana tunavumilia ndiyo kazi ndiyo maana mpaka leo tupo na timu. Vyovyote itakavyokuwa muhimu ni mimi kuwepo kazini basi maana tayari niko fiti nahitaji kufanya kazi.”
Beki Faustine Kulwa alisema uongozi uliwapigia simu baadhi ya wachezaji na kuwaahidi mambo mazuri kuanzia Jumatatu kwani kuna mwekezaji ataichukua timu hiyo, huku jitihada za Mwanaspoti kuupata uongozi wa klabu hiyo zikigonga mwamba.
“Watu wapo wa kucheza mechi kwa walioondoka ndiyo kama hivyo hali ni ngumu ya kiuchumi ila tunakomaa tu kazi inakuwa ngumu tuna matumaini mambo yatakuwa vizuri. Mimi nipo niliondoka kwa sababu nilikuwa nina majeraha nilikosa fedha ya kutibiwa,” alisema Kulwa.
Juhudi za kuupata uongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake mjini Musoma iligionga ukuta kwani simu zilikuwa zikiita bila kupokelewa.