Geita Gold inataka watano tu

SAFARI ya Geita Gold kurudi Ligi Kuu inazidi kupamba moto, huku uongozi wa klabu hiyo ukitamba unataka kutumia dirisha dogo kushusha wachezaji watano wa maana kuongeza nguvu kikosini ili kutimiza malengo ya kumaliza bingwa wa Ligi ya Championship na kupanda daraja.

Timu hiyo iliyoshuka msimu uliopita, inashika nafasi ya pili katika Ligi ya  Championship nyuma ya vinara Mtibwa Sugar kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa japo kila moja ina pointi 26 baada ya mechi 11.

Kocha Mkuu wa Geita, Amani Josiah aliliambia Mwanaspoti kuwa, tayari ameshawasilisha ripoti ya mahitaji ya usajili wa dirisha dogo kwenye uongozi wa klabu hiyo na sasa anasubiria majibu lengo likiwa ni kuongeza upana wa kikosi chake na kuhimili ushindani.

“Tumewapa uongozi ripoti ambayo tunasubiri kufanyiwa kazi. Mahitaji yetu ni wachezaji wachache tu kwa maana ya kuwa na kikosi kipana kwa ajili ya raundi ya pili,” alisema Josiah aliyeshinda tuzo ya kocha bora wa  Oktoba katika ligi hiyo.

Akizungumzia usajili huo, Mkurugenzi wa Mashindano Geita Gold, Liberatus Pastory alikiri kupokea ripoti hiyo ambayo inahitaji wachezaji wasiozidi watano katika nafasi ya kipa, beki wa kushoto, mshambuliaji na kiungo.

“Kwa sasa tunajikita zaidi katika michezo yetu mitatu kabla ya dirisha kufunguliwa baada ya hapo tutaanza kazi. Tunahitaji kuleta watu wa kazi hatusajili kwa ajili ya majaribio ndiyo maana hata usajili wetu wa dirisha kubwa ulikuwa sawa na Ligi Kuu,” alisema Pastory na kuongeza;

 “Kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi ni lazima kuna wachezaji wataondoka na hapa tutampa nafasi mwalimu afanye maamuzi kulingana na wachezaji anaowataka kwenye maeneo aliyosema ili apendekeze wachezaji wa kupisha hao wapya.”

Related Posts