African Sports watoa visingizio Championship

KOCHA Mkuu wa African Sports ‘Wanakimanu manu’, Abdallah Kessy ametoa sababu zinazowakwamisha kupata matokeo mazuri katika Ligi ya Championship, huku akisisitiza bado hajaikatia tamaa timu hiyo kwani anaamini mechi zilizosalia wanaweza kujikomboa na kuepuka kushuka daraja tena.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Muungano wakilibeba kombe msimu wa 1988, kwa sasa ipo nafasi ya 11 ikikusanya pointi saba lica ya kucheza mechi 11, ikishinda mbili na kutoka sare moja, huku ikipokea vipigo mara nane.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kessy amekiri kitendo cha kuutumia Uwanja wa Manungu,  Turiani Morogoro kama wa nyumbani umewaathiri ukizingatia na hali ya kiuchumi ambayo klabu hiyo inayozidi kuwaweka pabaya zaidi.

Kocha huyo amesema ushindani wa timu zinazoshiriki Ligi ya Championship msimu huu unategemeana zaidi  na uimara wa kiuchumi, ilihali wao wapo choka mbaya na kuzidi kuwapa ugumu licha ya kuwa na wachezaji bora.

“Sio siri ligi ni ngumu, lakini kitendo cha kutokuutumia uwanja wa nyumbani wa Mkwakwani kimetuathiri sana, ukizingatia na hali ya kiuchumi klabu zinapambana na hali hii, ila bado tuna imani tutapambana kutoka hapa tulipo,” alisema Kessy.

Timu hiyo ilirejea katika ligi hiyo baada ya misimu miwili kushuka hadi First League, lakini ni kama bado haijaizoea ligi hiyo kwa matokeo inayowaweka katika janga la kushuka daraja kurudi ilipotoka.

Kessy alisema licha ya matokeo na nafasi waliopo bado wanaendelea kuamini watafanya kweli wakianza na mechi ya leo dhidi ya Bigman ili kujinasua eneo la hatari.

Alisema lengo lao ni kuzitafuta nafasi tano za juu na kwamba wanasubuiri dirisha lifunguliwe Jumapili hii ili waongeze majembe ya kuwanusuru walipo kwani mechi zilizosalia ni nyingi za kuweza kupindua meza kama watakaza buti.

Kocha Kessy alisema katika dirisha hilo wataongeza wachezaji wasiozidi watano wakiwamo mmoja eneo la beki na kiungo, huku ushambuliaji atawabeba watatu kuarahisishia kazi.

Related Posts