Askofu awafunda Lissu, Mbowe na wafuasi wao

Askofu wa Kanisa la Uamsho la Moravian Tanzania, Emmaus Mwamakula amesema sasa ni wakati wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuionyesha dunia kwamba ndiyo chama kinachoweza kuiongoza nchi hii katika kuweka na kusimika mifumo ya utawala wa haki katika uchaguzi wake wa ndani.

Ameeleza hayo katika waraka aliouchapisha katika ukurasa wake wa Facebook, siku moja baada ya makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kutantagaza kuwania uenyekiti wa chama hicho, akitarajiwa kumvaa mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe.

ASKOFU ATOA KAULI JUU YA LISSU KUTAMKA KUGOMBEA UENYEKITI WA CHADEMA TAIFA!

Kipindi cha miezi ya hivi karibuni kumekuwepo na joto la uchaguzi ndani ya Chadema na joto limezidi kukua baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kutangaza nia yake ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Taifa jana tarehe 12 Desemba 2024.

Kwa kiasi fulani, nimekuwa karibu na viongozi wa Chadema katika ngazi mbalimbali na hasa walipoonewa na haki zao zilipofinywa, kuporwa na kukanyagwa na mamlaka. Hakuna asiyejua kuwa nilizunguka pia na Lissu nchi nzima wakati alipokuwa Mgombea wa Urais na kuwa nilihatarisha maisha yangu pia nilipoitangazia dunia kuwa maisha yake yalikuwa hatarini na hatimaye akaondoshwa nchini kwa msaada wa Ubalozi mmojawapo.

Hakuna mtu asiyejua kuwa wakati Mbowe alipokuwa gerezani nilihatarisha maisha yangu kwenda mahakamani kila wakati ikiwemo hata kufanya mengine ambayo hayaandikiki. Lakini nimekuwa karibu na viongozi na wanachama wengi wa Chadema kupitia utetezi wangu kila walipopata shida ya kuonewa, kutekwa na hata kupotezwa.

Ni wazi kuwa katika mazingira hayo, na mimi niliweza kulilipa gharama kubwa na pengine hata kuzidi gharama iliyolipwa na baadhi ya niliowatetea. Kwamba gharama hiyo haikulipwa na mimi tu, bali ililipwa pia na wengine wengi ambao walijitokeza katika kuwatetea. Kwa hiyo dhamira inatusuta na kutulazimisha kusema kila tunaopogundua au hata kuhisi kuwepo kwa dalili ufinyaji wa haki ndani ya jamii au chama ambacho tumekuwa karibu sana kukitetea pale kinapohujumiwa.

Askofu wa Kanisa la Uamsho la Moravian Tanzania, Emmaus Mwamakula

Moyo wangu uko na pia umelalia kwenye haki. Kwa hiyo sina maslahi yoyote ya kudumu ndani ya Chadema na chama chochote cha siasa isipokuwa kuona haki na utulivu vinatamalaki. Kama mambo hayo yanaanza kutoweka, ndipo sauti yangu inasikika na pia sitaweza kutulia. Katika wito huu sijawahi kuwa na maslahi au faida yeyote ya maana isipokuwa furaha ya moyo wangu kuona watu nilioshiriki kuwatetea wanaendelea vizuri (3 Yohana 1:1-4).

Ni wajibu wangu kujitokeza kusema mambo magumu katika jamii ambayo watu wengine huogopa kusema hasa kwa kuwa hayaongezi heshima kwa msemaji zaidi ya kumpunguzia heshima (kama aliwahi kuwa nayo hata hivyo).

Lakini kuhusu Uchaguzi wa Mwenyekiti ndani ya Chadema. Ninawiwa kusema mambo haya:

Kwamba huu sasa ndio wakati wa Chadema kuuonyesha ulimwengu kuwa wao ndio chama cha siasa chenye uwezo wa kushika dola hata kuiongoza nchi hii katika kuweka na kusimika mifumo ya utawala wa haki inayokosekana.

Chadema lazima kiendeshe Uchaguzi wa haki, ulio huru na wazi kwa mujibu wa katiba yake. Wagombea wote lazima waendeshe kampeni za staha na haki na bila vitisho kwa wagombea wengine. Wagombea au viongozi wote wa juu wa Chadema wanapaswa kukemea vitendo vya udhalilishaji wa mitandaoni unaofanywa na wafuasi na hata viongozi dhidi ya wagombea au timu za wagombea kupitia magrupu yao ya chama katika majimbo, mikoa, kanda.

Viongozi, wagombea pamoja na wanachama wa Chadema kwa ujumla lazima watambue ya kuwa kugombea nafasi yeyote ndani ya chama chao sio hisani ya baadhi ya watu au makundi na pia sio uhaini dhidi ya watu au kundi lolote.

Kumsuta na kumshambulia kwa sababu yeye ametangaza nia kugombea ni udikiteta ambao hauna tofauti na kumshinikiza Mbowe kuwa apumzike kwa kuwa ameongoza muda mrefu. Kuwasema na kuwanyanyapaa watu ambao wako upande wa Lissu au Mbowe ni udikiteta na haina tofauti na vitendo vya wasiojulikana ambao humteka na kumpoteza hata kumuua mtu aliye kinyume na mtu wao.

Ninawaza haya makundi yanayoporomosha matusi mitandaoni na kudhalilisha wenzao eti kwa sababu tu wanaunga mkono mgombea huyu au yule. Je, hao watu wanaoongoza na kuratibu makundi hayo, wangekuwa na silaha na mifumo kama ya wanaoratibu magenge ya watu wasiojulikana si nao wangeua zaidi?

Sisi ambao tuliwakimbilia na pia tunaoendelea kuwakimbilia kwa ajili ya kuwatetea, kuwapazia sauti na hata kuwatia moyo; hatujalala usingizi katika hili. Tunafuatilia kwa karibu sana juu ya hayo yanayoendelea. Ukifika wakati kama sisi tutaona ukiukwaji wa haki, kanuni, taratibu na katiba katika Uchaguzi huu wa viongozi wakuu Chadema tutatoka hadharani na tutawasema wanaokiuka bila kupepesa macho.

Kadharika, vijana ndani ya Chadema ambao wamepewa fursa ya kuangalia usalama wa viongozi ndani ya chama chao katika ngazi zote wanapaswa kujua kuwa wao wana wajibu wa heshima sana. Kwa hiyo, wasitumike na pia wasitumiwe katika kutukana, kuchafua na hata kudhalilisha viongozi au wagombea kwani hilo silo jukumu lao.

Askofu Mwamakula anawasihi sana vijana wa hamasa kuendelea na wajibu wao uliotukuka na kamwe wasikubali kuingizwa katika upambe wa kisiasa. Askofu anajua nafasi ya vijana hao na anaiheshimu na wasijiingize na wasiingizwe katika matusi dhidi ya wagombea wengine.

Ninatarajia kuona ukomavu wa kisiasa kupitia Uchaguzi wa nafasi ya Uenyekiti wa Chadema kwani ukomavu huo ni wa muhimu sana katika demokrasia yetu changa. Kwa kawaida, katika nchi zote watu hawatarajii kuona ukomavu wa kisiasa kutoka katika chama tawala, bali kutoka vyama vya upinzani na hasa chama kikuu cha upinzani ambacho ndiyo serikali tarajiwa.

Kupitia Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Watanzania ndio watapima kama chama hicho kimekomaa kupewa uongozi wa dola au la. Hii ni fursa ya kipekee sana kwa chama hiki.

Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?

Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!

Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula

Dar es Salaam, 13 Desemba 2024; saa 5:20 asubuhi

Related Posts