Aliyezini na wanawe, kuwaambukiza kaswende atupwa jela miaka 30

 Mwanza. Ni kazi ya ibilisi? Ni swali la kujiuliza baada ya kuthibitika kuwa baba mzazi wa watoto watatu wa kike wakiwemo pacha, alifanya nao mapenzi na kuwaambukiza ugonjwa wa kaswende.

Kosa alilolitenda mkazi wa Kijiji cha Gweli katika wilaya ya Sengerema, linaangukia katika kifungu cha 158 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, kinachozuia kufanya ngono na ndugu wa damu (maharimu) na adhabu yake ni kutumikia kifungo cha miaka 30 jela ambacho amehukumiwa.

Kifungu hicho kinasema mwanaume yeyote ambaye amekatazwa kufanya ngono na mwanamke anayemjua ni mjukuu wake, binti yake, dada yake au mama yake, mwanaume huyo atakuwa amekosa na akipatikana na hatia atastahili adhabu.

Pia, Kifungu kidogo cha (2) kimeeleza haitakuwa ni utetezi kuwa kitendo cha ngono kilifanywa kwa ridhaa ya mwanamke huyo na wala kosa hilo haliangukii katika kosa la kubaka.

Katika kesi ya rufaa nama 640 ya 2021 iliyotolewa hukumu Desemba 12, 2024 na majaji watatu jijini Mwanza, mwananme huyo alianza kuwafanyia wanae ukatili huo Januari 5, 2019 saa 4:00 usiku.

Wanawe hao ni pacha waliokuwa na umri wa miaka 15 na mmoja aliyekuwa na umri wa miaka 12. Aliendelea kufanya nao ngono kwa muda mrefu na ilipobainika na kupimwa, walikutwa wameambukizwa ugonjwa wa zinaa.

Ushahidi uliotolewa unaonyesha kuwa mrufani huyo alikuwa akiishi na wanawe katika nyumba yenye vyumba viwili na katika chumba kimojawapo, kulikuwa na kitanda cha ngazi walichokuwa wakitumia kulala baba na wanawe.

Wakati watoto wake hao walikuwa wanalala kitanda cha juu, mrufani alikuwa analala kitanda cha chini na usiku wa Januari 5, 2019, alimwamsha mmoja wa watoto hao na kumlazimisha afanye naye ngono.

Hakuishia hapo, Septemba 21, 2019 na Mei 9, 2020, aliwageukia wengine wawili na kuwalazimisha kufanya ngono na akaendelea kuwafanyia ukatili huo mara nyingi, ambazo watoto hao walishindwa kuzihesabu.

Ukatili huo ulipogundulika ukatolewa taarifa polisi ambapo mshtakiwa alikamatwa na kushtakiwa kwa makosa sita, mawili ya kuwabaka wanawe na matatu ya kuzini na watoto wake wa kuzaa.

Katika utetezi wake katika Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, mrufani aliyekuwa na umri wa miaka 45 wakati kesi hiyo ikinguruma, alikiri kuwafahamu kuwa ni watoto wake wa kike na ni damu yake.

Akaeleza tarehe zinazotajwa na mashahidi, alikuwepo nyumbani na familia yake hiyo, lakini hakuwahi kufanya vitendo vya ngono na wanawe.

“Tarehe 5.01.2019 muda wa saa 4:00 usiku nilikuwa nyumbani na familia yangu lakini sikuwahi kufanya ngono na mtoto wangu (anamtaja) na wala sijawahi kufanya mapenzi na hao wengine (anawataja) ni tuhuma za uongo,” alijitetea.

Aliendelea kujitetea mahakamani kuwa “wala sijawahi kuugua ugonjwa wa kaswende na ninashangaa namna hawa watoto wangu wote walivyougua huu ugonjwa. Nadhani ni ugonjwa tu na sijui ulitokea wapi.”

Katika hukumu yao, majaji hao, Rehema Kerefu, Abraham Mwampashi na Dk Eliezer Feleshi, waliitupa rufaa ya mwanamme huyo na kusisitiza kuwa shtaka la kufanya mapenzi na watoto wake wa damu lilithibitishwa na mahakama za chini.

Mwanamme huyo ambaye jina lake tunalihifadhi ili kuwalinda watoto hao, awali alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, lakini alipokata rufaa Mahakama Kuu, kifungo kikaongezwa hadi miaka 30 jela.

Hata hivyo, hakuridhika na akakata rufaa mahakama ya rufani akiegemea hoja tatu ikiwamo kwamba kutiwa kwake hatiani na kufungwa kulitokana na utetezi dhaifu alioutoa na si kutokana na uzito wa ushahidi wa Jamhuri.

Pia alijenga hoja kuwa mahakama za chini zilikosea kisheria zilipoona ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa pili ambao ni wanawe ulikuwa wa kuaminika na kwamba alitiwa hatiani na kufungwa kwa kuegemea hukumu iliyokiuka sheria.

Majaji hao walisema kwa kuchambua ushahidi uliopo katika jalada, yapo mambo matatu aliyoyabaini ambayo mahakama ya chini iliyabaini.

“Mambo matatu aliyoyagundua ni kuwa shahidi wa tatu hakuingiliwa bali aliambukizwa kaswende, kwa hiyo hakimu akalifuta shtaka la kubaka na kulibadili na kuwa la kujaribu kubaka,” walisema majaji hao katika hukumu yao.

“Hakimu alibaini ushahidi wa utetezi wa mshtakiwa ulikuwa dhaifu usingeweza kuporomosha ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri na kuwa mahakama ilimtia hatiani kwa makosa aliyopatikana nayo na hatia na kupewa adhabu.”

Kuhusu madai kuwa ushahidi wa wanawe wawili ulikuwa si wa kuaminika, majaji hao walisema hakuna ubishi na ni jambo ambalo halikubishaniwa kuwa mrufani ni baba wa watoto hao na walikuwa wakilala nyumba moja na kitanda kimoja.

Majaji hao walisema simulizi za watoto wake hao kwa upande mmoja na simulizi ya mrufani kwa upande wa pili, unathibitisha uwepo wa ngono iliyokatazwa na kusisitiza kuwa ushahidi wa wanawe hao ni wa kuaminika pasipo na shaka.

Mbali na hilo, majaji hao walisema ushahidi wa watoto wake hao uliunganika na ule wa mashahidi namba 4 na 5, hivyo rufaa hiyo haina mashiko, inatupwa na mshtakiwa ataendelea kutumikia kifungo hicho cha miaka 30 jela.

Related Posts