Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Benki
ya Dunia imeshangazwa na hatua kubwa iliyofikiwa na Serikali katika
kutekeleza Mradi wa Kimkakati wa Reli ya Kisasa wa SGR, na kuahidi kuwa
itaweka mkono wake kusaidia ujenzi wa Reli hiyo muhimu kwa kukuza
biashara na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kauli
hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam, na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika
wa Benki ya Dunia anayesimamia Ujenzi wa Miundombinu, Bi. Wendy Hughes,
aliyepo nchini kwa ziara ya kikazi, alipokutana na kufanya mazungumzo na
Mawaziri watatu wa Kisekta, wakiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt.
Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa na
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. Abdallah Ulega.
Bi.
Hughes aliyeambatana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan
Belete na Viongozi wengine waandamizi wa Benki hiyo, alisema kuwa
amesafiri kwa kutumia reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na
kushangazwa na kiwango cha ubora wake wa viwango vya kimataifa.
Alisema
kuwa Benki ya Dunia inaendelea kuchakata maombi yaliyowasilishwa na
Serikali katika Benki hiyo, na kwamba iko tayari kusaidia ujenzi wa Reli
hiyo ya Kimkakati na kushauri pia sekta binafsi ishirikishwe kikamilifu
kuhakikisha kuwa malengo ya kuanzishwa kwa mradi huo yanafikiwa kwa
ufanisi mkubwa.
Wakizungumza
katika kikao hicho kuhusu Mradi wa SGR, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt.
Mwigulu Lameck Nchemba, na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Profesa Makame
Mbarawa, waliishukuru Benki ya Dunia kwa kuamua kutoa fedha za kujenga
mradi huo ambao umefikia hatua mbalimbali za ujenzi na ni mfano Barani
Afrika na Duniani kwa ujumla
Walieleza
kuwa Mradi wa SGR unaogharimu zaidi ya shilingi trilioni 10 za
Tanzania, ni muhimu katika kuimarisha biashara na usafirishaji wa abiria
na mizigo si tu kwa Tanzania, bali katika nchi za Ukanda wa Maziwa
Makuu, ambapo biashara kati ya nchi hizo inatarajiwa kuongezeka na
kusaidia kutatua tatizo la ajira kwa wananchi.
Mkutano
huo uliowashirikisha Wakuu wa Taasisi katika Sekta ya Usafirishaji na
Ujenzi, ulikuwa na ajenda tatu ikiwemo ujenzi wa Mradi wa Mabasi
yaendayo haraka Jijini Dar es Salaam-BRT, Mradi wa Reli kwa Kiwango cha
Kimataifa-SGR na namna ya kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza
miradi kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi-PPP.
Waziri
wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akilakiana na Mkurugenzi wa
benki ya Dunia, anayesimamia Miundombinu, Bi. Wendy Hughes, alipofanya
ziara ya kikazi nchini, ambapo Mkurugenzi huyo alikutana na kufanya
mazungumzo na Mawaziri watatu wa Kisekta, akiwemo Waziri wa Uchukuzi,
Prof. Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. Abdallah Ulega,
ambapo walijadili kuhusu Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka-BRT, Ujenzi wa
Mradi wa Treni ya Mwendo Kasi (SGR), na namna ya kuiwezesha sekta
binafsi kwa kushirikiana na Sekta ya Umma kushiriki katika utekelezaji
wa miradi ya maendeleo.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha- Dar es Salaam)