Dar es Salaam. Siku moja baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu kutangaza nia ya kuwania uenyekiti, mwanasiasa mkongwe, Profesa Abdallah Saffari amesema amefurahishwa na uamuzi huo, lakini amempa tahadhali kuelekea mchakato huo.
Amesema kwa uzoefu wake wa siasa za Tanzania, mara nyingi ni vigumu kuwashinda wenyeviti waliopo madarakani kwa sababu mbalimbali, akijitolea mfano wake namna alivyopambana na Profesa Ibrahim Lipumba katika uchaguzi wa CUF mwaka 2009 kuwa alipachikwa kila aina ya majina likiwamo la pandikizi.
Jana Alhamisi Desemba 12, 2024, Lissu aliutangazia umma kuhusu dhamira yake ya kuwania uenyekiti wa Chadema, katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka 2025.
Katika mkutano huo wa jana, Lissu alisema kwa mazingira ya saisa za sasa, Chadema inahitaji kuwa na mwenyekiti wa kariba yake, ndiyo maana amefikia uamuzi huo.
Ingawa hadi sasa, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe hajaweka wazi kama atawania tena nafasi hiyo, lakini Lissu alisema, “kwa msimamo wangu thabiti na usiotetereka, ninazo sifa na uwezo wa kusimamia maboresho ya chama chetu katika kipindi hiki kigumu.”
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Desemba, Profesa Safari amesema hatua ya Lissu ambaye waliwahi kufanya kazi wote Chadema, ni nzuri itakayoleta ushindani kwenye uchaguzi huo.
Profesa Saffari ambaye ni mbobevu kwenye masuala ya sheria, amesema huenda Lissu amechoshwa na kinachoendelea ndani ya chama chao, ndiyo maana ameamua kuwania nafasi hiyo ya uenyekiti.
Hata hivyo, amesema anapaswa kujiandaa kwa sababu atakabiliana na watu aliowaita ‘machawa’ watakaofanya kila linalowezekana ili kada huyo asishinde kwenye kinyang’anyiro hicho.
“Lazima kuwepo na mabadiliko ya uongozi, kama nilivyowahi kusema kule CUF, kwamba usultani na ufalme haufai. Kwa hiyo acha tuone vumbi litimke, tuonane sura zetu vizuri.”
“Nimefurahi sana, naona historia inajirudia, kwangu mimi na Frederick Sumaye (Waziri mkuu mstaafu). Sioni kitu kibaya kwa Lissu kugombea, hata mimi niligombea nikiwa CUF,” amesema Profesa Saffari.
Akisimulia kisa chake, alisema: “Nakumbuka sikuwa na cheo chochote, nilikuwa mshauri wa sheria lakini nilipoamua kugombea uenyekiti CUF ikaanzishwa kampeni kwamba Saffari ni pandikizi, na mtani wangu Profesa Lipumba alikaa kimya, hakusema kitu. Wakati wa uchaguzi waliwachukua wapiga kura na kuwaweka sehemu moja na kuwaeleza Saffari pandikizi,” amesema.
Profesa huyo amesema baadhi ya watu wake wa karibu nao walimgeuka kwa sababu tu anataka uenyekiti.
“Kisa, walidhani nitanyooka na kudai tume huru, wakanipiga vita, watu wakaaminishwa kwa kulishwa matango pori, niliambulia kura sita tu kwenye uchaguzi ule,” amesema Profesa Saffari.
Kutokana na hilo, mtaalamu huyo wa sheria, aliyewahi pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema (bara), amemtaka mwanasheria mwenzake Lissu kuelewa hali hiyo, akisema mifano hai ipo kwa watu waliojaribu kuutaka uenyekiti na kilichowapata.
Kwa mujibu wa Profesa Saffari, aliwania uenyekiti wa CUF, ili kuleta ushindani na kuondoa mwenendo wa viongozi kukalia kiti hicho kwa kipindi kirefu, jambo aliloliita kuwa ni sawa na usultani.
“Waliniita pandikizi, ujinga sana ule, yaani pandikizi ningefukuzwa kazi? Lissu lazima alijue hili. Lissu ana heshima kubwa, watu wanampenda, lakini ajue kuna madhila yaliyomkuta Sumaye pia (Frederick –waziri mkuu mstaafu),” amesema.
Mwaka 1999 Profesa Saffari aliyewahi kuwa mkurugenzi wa masomo na mipango wa Chuo cha Diplomasia, jijini Dar es Salaam, alifukuzwa kazi kwa kosa la kumtetea kisheria Profesa Lipumba na wenzake, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kupitisha muda, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyikia viwanja vya Zakhem Mbagala.
Huku akiangua kicheko, Profesa Saffari amemkumbusha Lissu kwa kumtolea mfano wa Sumaye, aliyewania uenyekiti wa Chadema Pwani, lakini “kilichompata kila mtu na dunia ilishuhudia.”
Katika uchaguzi huo, Sumaye aliyehamia Chadema mwaka 2015, kisha kurejea tena CCM, alikuwa mgombea pekee lakini alipigiwa kura za Hapana 48 dhidi ya 28 za Ndiyo na hivyo akaanguswa.
Inaelezwa kuwa hatua hiyo ilimrudisha nyuma Sumaye ambaye pia aliwahi kuwa mbunge wa Hanang’ mkoani Manyara na inadaiwa, alikuwa na nia ya kuutaka uenyekiti wa Taifa wa Chadema.
“Sasa huyu ndugu yangu (Lissu) ajiandaee na achukulie mfano wangu na Sumaye. Kuna watu walimshughulikia Sumaye,” amesema Profesa Saffari.
Mbali na hilo, Profesa huyo amekumbushia namna alivyoshambuliwa na watu aliowaita ‘machawa’ wa viongozi kutokana na msimamo wake wa kuitaka Chadema isishiriki uchaguzi Mkuu wa 2020.
“Kuna chawa wa viongozi walinitukana na kuniambia nasema uongo, walinitukana sana, nikamwambia Dk Mashinji (Vincent-katibu mkuu wa zamani wa Chadema, sasa ni mkuu wa wilaya), hawa jamaa wananitukania nini?” amesema.
Kutokana na hilo, Profesa Saffari amesema, licha ya sifa nzuri alizonazo Lissu, baadhi ya watu wataanza kumshughulikia kwa kumtusi pia.
Huyu ndiye Profesa Saffari
Kwa sasa Profesa Saffari mwenye misimamo na sifa ya kusimamia ukweli ameachana na siasa, amejikita kwenye utunzi wa vitabu kama njia nyingine ya kuendeleza harakati zake za ukombozi.
Profesa Saffari aliyebobea kwenye sheria, alijizolea umaarufu kupitia utunzi na uandishi wa vitabu vikiwemo cha “Mashtaka ya Jinai na Utetezi” kinachotumika katika vyuo vikuu na Shule Kuu ya Sheria kufundishia mwenendo wa mashtaka ya jinai.
Mbali na sheria, Profesa Saffari ni mtaalamu wa Kiswahili na ameandika vitabu mbalimbali kama “Harusi” ambacho kimetumika kama rejea katika shule za sekondari nchini.
Pia ameandika riwaya za “Kabwela” cha mwaka 1978, “Joka la Mdimu”, “Piga Bongo na kitabu cha “Nahau za Kiswahili.”