Zambia. Mahakama ya Katiba ya Zambia imemua kuwa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Edgar Lungu hawezi kugombea kwenye uchaguzi wa 2026 kwa kuwa tayari amehudumu mihula miwili.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari ka AP, mahakama imesema muda ambao Lungu alihudumu kama Rais wa taifa hilo kati ya 2015 na 2016 kufuatia kifo cha Michael Sata, kinahesabiwa kama muhula kamili.
Lungu alishinda uchaguzi kwa muhula wa pili kuanzia 2016 hadi 2021 lakini mwaka uliopita, alitangaza kujitosa tena akilenga kugombea dhidi ya Rais wa sasa, Hakainde Hichilema, kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Uamuzi wa jopo la majaji saba ulitangazwa moja kwa moja kwenye televisheni na radio za taifa na mamilioni walikuwa wakifuatilia uamuzi huo, kwa mujibu wa Shirika la Utangaza la Sauti ya Amerika (VOA).
Lungu alishindwa na Hichilema katika uchaguzi wa 2021 hivyo uamuzi huo uliotolewa Jumanne una maana kwamba hataweza kushiriki kwenye uchaguzi huo.
Lungu alichaguliwa kuwa Rais kwa mara ya kwanza Januari 2015 kumalizia miezi 20 iliyosalia ya muhula wa mtangulizi wake Rais Sata, aliyefariki akiwa madarakani Oktoba 2014.
Hata hivyo, alitaka muda huo usihesabiwe kwa kuwa hakuhudumu kwa muhula mzima wa miaka mitano.
Kufuatia hatua hiyo mwezi uliopita, Lungu alichaguliwa na muungano wa upinzani wa Tonse kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi wa 2026 ili kushindana na Rais Hichilema.
Aidha, akijibu uamuzi huo wa Mahakama, Lungu mwenye miaka 68 amesema umeghubikwa na mkono wa kisiasa.