Mchengerwa: Tutamega maeneo ya hifadhi za asili kwa shughuli za maendeleo

Rufiji. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ametangaza dhamira ya kutaka maeneo ya hifadhi za asili kumegwa kwa ajili ya makazi na shughuli za maendeleo ya wananchi.

Mchengerwa ameyataja maeneo hayo kuwa ni Msitu wa Kale na Sameroji katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Waziri huyo ametoa kauli hiyo leo Desemba 13, 2024 wakati akipokea msaada wa vifaatiba vyenye thamani ya zaidi ya Sh12 milioni kutoka Benki ya NMB kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Rufiji na baadhi ya vifaa hivyo vimeabidhiwa kwa wajawazito.

“Nimezungumza na Waziri wa Utalii kuhusu makubaliano tuliyofanya mwaka 2018. Tumekubaliana maeneo ya Kale na Sameroji yaongezwe kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa Utete kufanyia shughuli zao,” amesema.

Amesema uamuzi huu umechangiwa na mpango wa kuitanua wilaya hiyo ili kufungua fursa mpya za kiuchumi na kimaendeleo kwa wananchi.

Mbali na hilo, Waziri Mchengerwa ameuagiza uongozi wa wilaya hiyo kuangalia uwezekano wa kuanza kujenga uwanja wa ndege katika eneo la Ngarambe ili itarahisisha usafiri na usafirishaji.

“Lengo letu ni kunyanyua uchumi wa wananchi. Naomba wakazi waanze kujenga nyumba za biashara, kwani wageni wataanza kufurika wilaya hii kwa wingi katika siku zijazo,” amesema.

Awali, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Seka Urio amesema msaada huo wa vifaatiba ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kuunga mkono Serikali katika kutatua changamoto zinazokumba jamii, hasa za sekta ya afya.

“Hii ni kawaida yetu kutenga asilimia moja ya faida yetu kila mwaka kurudisha kwa jamii, na leo tumekabidhi mashuka 300 na seti 300 za vifaa vya wajawazito, vyote vyenye gharama ya Sh12 milioni,” amesema Urio.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Michael Mkungwa amesema utasaidia kupunguza changamoto za vifaa vya kujifungulia ambazo zimekuwa zikihitaji usaidizi wa haraka.

“Vifaa hivi serikali imekuwa ikivitoa bure, lakini bajeti haiwezi kukidhi mahitaji yote. Hii ni hatua nzuri sana kwani itapunguza changamoto kwa wajawazito,” amesema Dk Mkungwa.

Mmoja wa wajawazito waliopokea msaada huo, Mwatano Tindwa, mkazi wa Kata ya Utete, ameeleza kuwa msaada huu umempunguzia mzigo wa kiuchumi.

“Iwapo ningenunua vifaa hivi dukani, ningetumia Sh50, 000 kwa seti nzima, hii ni faraja kubwa kwangu,” amesema Mwatano.

Related Posts