Mpox yaendelea kuenea nchini Kenya – DW – 13.12.2024

Miji yenye shughuli nyingi za usafiri hasa za kutoka nje ya nchi inaripotiwa kuathiriwa zaidi nchini huku Wakenya wengi wakikosa taarifa muhimu kuhusu ugonjwa huo. 

Wizara ya afya ya Kenya imethibitisha wagonjwa wapya waliokutwa na ugonjwa wa mpox, hatua ambayo inafikisha jumla ya wagonjwa waliothibitishwa kupata ugonjwa huo kuwakatika kaunti 12 nchini kote.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Waziri wa afya daktari Deborah Barasa amesema visa hivyo vipya vimeripotiwa katika kaunti mbili, vitatu vikirikodiwa mjini Nakuru na viwili mjini Mombasa, pwani ya Kenya.

Jopo la WHO lasema mpox bado ni kitisho cha afya duniani

Waziri Barasa amesema tangu kuthibitishwa kwa ugonjwa huo nchini mwezi Julai mwaka huu zaidi ya wasafiri milion 2.2 wamechunguzwa kwenye sehemu za mipaka mbalimbali nchini Kenya.

Kufikia sasa maabara ya kitaifa ya umma imepokea sampuli 322 za kufanyia vipimo. Sampuli 28 zilibainika kuwa na ugonjwa huo na zingine mbili zinasubiri kufanyiwa uchunguzi wa kina. Kati ya wagonjwa 28 waliopatikana na ugonjwa wa mpox, mmoja amefariki, wanane wanaendelea kutibiwa, wawili wamejitenga na 17 wameshapona.

Kenya yaweza kudhibiti Mpox

Kenya inasema ina nafasi nzuri ya kudhibiti ugonjwa huo. Mary Muthoni katibu mkuu wa afya ya umma anaeleza.

“Ni muhimu kutambua kwamba uchunguzi ni muhimu katika maeneo hayo ya mpaka ili tuepuke kufurika kwa watu ambao pengine wana dalili na dalili za ugonjwa unaokuja nchini bila kutambuliwa,” amesema Mary.

Chanjo ya dhidi ya Monkeypox yaanza kutolewa Goma

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Maafisa wa afya katika Kaunti ya Nakuru wamewekwa katika hali ya tahadhari kufuatia kuthibitishwa kwa visa vitatu vipya vya Mpox katika kaunti hiyo. Dereva wa lori aliyewasili kutoka Rwanda ni mmoja wa waliopatikana na ugonjwa huo.

Kulingana na Mkurugenzi wa Afya ya Umma Kaunti ya Nakuru Elizabeth Kiptoo, kama sehemu ya mkakati wa kukabiliana na maambukizi, wanafuatilia madereva wa masafa marefu na wametambua eneo hili kama lililo kwenye hatari kubwa ya maambukizi. Aidha wameanzisha vituo vya dharura vya afya ya umma ili kuratibu juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo, kuchukua hatua mbalimbali za haraka, kufuatilia mawasiliano na kuimarisha ufuatiliaji.

Tahadhari kwa umma

Serikali inasisitiza tahadhari. Wagonjwa wanaoshukiwa au kuthibitishwa kuwa na mpox mara nyingi huwekwa chini ya uangalizi wa karibu.

Wizara ya afya imesema inashirikiana kwa karibu na serikali za kaunti na wadau wengine kutoa uhamasisho kuhusu ugonjwa huo pamoja na umuhimu wa kuzingatia hatua zilizowekwa za kuuzuia maambukizi.

Virusi vya Mpox 2024 | Vipimo dhidi ya Mpox, ni njia muhimu kubaini maambukizi
Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa kukabili maambukizi ya Mpox, ni uhamasishaji kwa umma na wataalam kufanya vipimo vya kwa wanaoshukiwa kuambukizwa.Picha: Dado Ruvic/REUTERS

Hatua za kudhibiti maambukizi ni kama vile kuongeza uhamasishaji kuhusu dalili na njia za kukabiliana na ugonjwa wa mpox, kuepuka mawasiliano ya moja kwa moja na watu walio na dalili za ugonjwa, kuhimiza usafi wa mikono na kuimarisha mifumo ya huduma za afya.

Awali mkurugenzi mkuu wa afya Dr. Patrick Amoth alionya kuhusu aina iliopo ya mpox.

Amoth amesema “aina hii mahususi ya mpox inaitwa eclid 1B ambayo inaweza kuambukizwa zaidi na ni mbaya zaidi katika suala la muundo wa ugonjwa kwa hiyo ni muhimu zaidi kwetu kuelewa tunachopambana nacho.”

Kenya kama nchini nyingi za bara Afrika zimejifunza kutoka kwa janga la Uviko-19, na wametumia ujuzi huo wa dharura kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Kadhalika, ushirikiano wa kimataifa na mashirika kama vile Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, Africa CDC, na shirika la afya ulimwenguni WHO yametoa rasilimali na mafunzo maalum kuhusu namna ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko.

Related Posts