Akiwa ziarani nchini Uturuki siku ya Ijumaa (Disemba 12), Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken, alisema alikuwa anaona dalili za kupigwa hatua kuelekea makubaliano ya kusitisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza uliokwishabomolewa kabisa kwa makombora na mizinga ya Israel.
“Tumeijadili Gaza, na tumejadili fursa iliyopo ya kupata makubaliano ya kusitisha mapigano. Na tumeona kwamba ndani ya wiki chache zilizopita, kumekuwa na ishara za kutia moyo kwamba jambo hilo linawezekana.” Alisema Blinken baada ya mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uturuki, Hakan Fidan.
Soma zaidi: Maafisa: Mashambulizi ya Israel yaua watu 28 Gaza
Kumekuwapo na uvumi kutokea Washington kwamba rais mteule wa Marekani, Donald Trump, ameagiza kwamba suala la Gaza liwe limemalizika kabla ya yeye kuingia rasmi madarakani mwezi ujao, hali inayoashiria kwamba wapatanishi wa kimataifa pamoja na pande zote zinazohusika na hali inayoendelea Gaza wana muda wa chini ya wiki tatu kuhakikisha kuwa vita vinasitishwa.
Marekani pamoja na mataifa kadhaa ya Magharibi ndio vinara wa uungaji mkono wa kijeshi, kifedha na kisiasa kwa Israel.
Israel yaendelea na mashambulizi Gaza
Kwenyewe Gaza, vyanzo kutoka mahospitalini vilisema mashambulizi ya anga ya Israel yamewauwa Wapalestina 30 na kuwajeruhi wengine wapatao 50 usiku wa kuamkia Ijumaa.
Familia kadhaa ambazo zimegeuka kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na miezi 14 ya mashambulizi, zilikuwa zimejihifadhi kwenye jengo moja la huduma za posta katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat, na mashambulizi hayo yaliifanya idadi ya waliouawa kwa siku nzima kufikia 66 kwenye Ukanda wa Gaza.
Soma zaidi: Israel yawafungulia mashtaka ya ugaidi Wapalestina watatu
Jeshi la Israel lilidai kwamba mashambulizi yake hayo yalimlenga mwanachama wa ngazi za juu wa kundi la Islamic Jihad, mojawapo ya makundi yaliyohusika na uvamizi wa Oktoba 7 mwaka jana dhidi ya Israel.
Hata hivyo, Israel haikulitaja jina la mwanachama huyo wa Islamic Jihad ambaye inadai anahusika na mashambulizi dhidi ya raia na wanajeshi wake, na ikisema kundi hilo linatumia miundombinu ya raia na wakaazi wa Gaza kama ngao kwa harakati zake.
Kambi ya wakimbizi ya Nuseirat ni mojawapo ya kambi nane za kihistoria kwenye Ukanda wa Gaza ambazo zimekuwa zikiwahifadhi Wapalestina tangu mwaka 1948.
Kwa sasa, ni sehemu ya mojawapo ya maeneo yenye idadi kubwa sana ya watu, kwani maelfu ya waliokimbia maeneo mengine ya Ukanda hao wamejihifadhi hapo.
Vyanzo: AFP, Reuters