Meneja Mawasiliano na Uhusiano EWURA, Bw.Titus Kaguo, akitoa elimu ya udhibiti wa huduma za nishati na maji wakati wa mafunzo hayo.
…..
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) leo Tar.13 Desemba 2024, imefanya mafunzo kwa Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) jijini Dar es Salaam, huku msisitizo ukiwa kwenye uvunaji wa maji ya mvua katika kukabiliana na upungufu wa huduma za maji katika maeneo mbalimbali.
Pia katika mafunzo hayo mkazo umetolewa katika kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia na kwenye magari.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Bw. Titus Kaguo, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Dkt. James Andilile, alisema lengo la mafunzo ni kuwajengea uwezo wanahabari kutoa taarifa za sekta ya nishati na maji kwa usahihi na kwa wakati kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Pamoja na uhamasishaji wa uvunaji maji ya mvua na matumizi ya nishati safi, mafunzo hayo pia yalijikita katika historia ya EWURA, shughuli za udhibiti wa sekta za umeme, petroli, gesi asilia na maji pamoja na mafanikio ya udhibiti tangu kuanzishwa kwa EWURA mwaka 2006.
Naye Katibu wa JOWUTA Bw. Suleiman Msuya aliishukuru EWURA kwa mafunzo hayo huku akitoa rai kwa waandishi wa habari kutumia elimu walioipata kutoa taarifa za nishati na maji kwa usahihi zaidi.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano EWURA, Bw.Titus Kaguo, akitoa elimu ya udhibiti wa huduma za nishati na maji wakati wa mafunzo hayo.
Kaimu Meneja wa Kanda ya Mashariki EWURA, Mha. Mwanamkuu Kanizio, akijibu swali kuhusu sekta ya umeme wakati wa mafunzi hayo.
Baadhi ya waandishi wa habari wanachama wa JOWUTA, wakifatilia kwa makini mafunzo hayo leo.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Bw. Titus Kaguo, aliyekaa katikati,akiwa katika katika picha ya pamoja na baadhi ya wanachama wa JOWUTA na waandishi wa habari waliohudhuria mafunzo hayo leo, Dar es Salaam.