Wasimulia dakika za mwisho kabla ya kubakwa, kuuawa mwanafunzi wa Rucu

Iringa. Wakati mwili wa mwanafunzi Rachael Mkumbwa ukitarajiwa kuzikwa kesho Jumamosi wilayani Ileje mkoani Songwe, waliokuwa wapangaji wenzake wameelezea dakika zake za mwisho kabla ya kukutwa na umauti.

Rachel aliyekuwa akisoma mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) mkoani Iringa, alikutwa amefariki dunia nyumbani kwake jana Desemba 12, 2024 kwa madai ya kubakwa hadi kuuawa.

Dorice Dimoso mpangaji mwenzake akizungumza na Mwananchi nyumbani kwao Mtaa wa Mhimba B, mjini Iringa leo Ijumaa Desemba 13, 2024, amesema waliishi na Rachael vizuri na hajawahi kutofautiana na mtu yeyote mtaani hapo.

Amesema hata siku ya tukio mwanafunzi huyo alirejea nyumbani mapema kutokea chuoni.

“Juzi alirudi nyumbani kwenye saa 9 hivi jioni na alikuwa mchangamfu tu kama siku zote, tukasalimiana naye na akaingia chumbani kwake, hatukujua kilichofuata kwa kuwa kila mmoja ana mlango wake,” amesimulia Dimoso.

Ameongeza: “Mimi ni mjasiriamali basi nikarejea kwenye shughuli zangu na niliporudi jioni hatukuonana,  tumekuja kushtukia ameuawa kifo kibaya,” amesema mpangaji huyo.

Naye Salimu Issa mpangaji katika nyumba hiyo anasema mara ya mwisho kuonana na Rachael walizungumza mambo kadhaa ya kawaida tu na baadaye waliagana akaingia chumbani kwake akafunga mlango.

Amesema kilichoendelea baadaye hafahamu alishutuka kuambiwa kwamba kauawa, huku akisisitiza labda Jeshi la Polisi likifanya uchunguzi kwa kina, litabaini sababu za mauaji hayo.

“Hatujawahi kusikia chochote ambacho tunaweza kuhisi labda ndiyo chanzo cha mauaji yake, tunachoomba ni kukamatwa kwa waliohusika ili sheria ichukue mkondo wake” amesema Issa.

Naye Diwani wa Makongoroni, Thadeus John akizungumza na Mwananchi amesema  wanasubiri taarifa rasmi za Jeshi la Polisi ambalo lilifika nyumbani kwa marehemu na kuuchukua mwili.

Hata hivyo, anasema taarifa za awali zinaonyesha mwanafunzi huyo mbali ya kuuawa, amebakwa pia.

“Hili ni tukio la tatu kutokea katika mtaa huu japokuwa mauaji hayalingani,” amesema diwani huyo.

Amesema wiki iliyopita waliokota maiti  ikiwa imefungwa kamba na kutelekezwa kwenye mtaro.

“Lakini kwa tukio la huyu mwanafunzi, tumesimuliwa na mwanafunzi aliyekuwa naye karibu kuwa waliachana naye saa 2 usiku na kila mmoja akaenda chumbani kwake kulala, ila aliposhutuka usiku akakuta ameibiwa simu mbili na laptop, akamfuata Rachael (marehemu) chumbani lakini kabla hajaufikia mlango akaona uko wazi na yeye amelala kifudifudi akiwa hana nguo hata moja na alikuwa tayari amekufa,” amedai diwani huyo.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ruaha (Ruco), Profesa Pius Mwageni licha ya salamu za pole kwa wanafunzi wenzake na jamii iliyokuwa ikiishi na marehemu huyo wakati wa kuuaga mwili huo leo chuoni hapo, amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa Polisi ili kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.

Amesema tukio hilo wanalikabidhi mikononi mwa Mungu akieleza kuwa ni msiba mkubwa huku akiwaasa wananchi kuendelea kutenda mema ili kuwa na mwisho mwema katika maisha ya dunia na mbinguni.

“Tutaendelea kumuombea kwa Mungu, ni huzuni na simanzi kubwa lakini tumshukuru Mungu kwa nafasi yake, yote tumkabidhi yeye, tuendelee kuombeana na kutenda mema” amesema Profesa Mwageni.

Katika taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani Iringa leo Desemba 13, 2024 na Kamanda wake, Allan Bukumbi imeeleza kuwa marehebu alibakwa kisha watuhumiwa wakachukua simu yake ya mkononi.

“Tukio hili lilitokea Desemba 12 saa 5 usiku, ambapo upelelezi umebaini watuhumiwa waliingia chumba cha jirani ambaye naye ni mwanafunzi nako wakachukua simu mbili na laptop,” amesema kamanda huyo.

Kamanda huyo ametoa wito kwa wanaanchi na mtu yeyote mwenye taarifa za  kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu hao, wasisite kuziwasilisha ili zifanyiwe kazi.

Related Posts