‘Marufuku kuwakatia maji wateja ‘wikiendi’

Dar es Salaam. Mamlaka za maji nchini zimezuiwa kukatia wateja wake huduma za maji mwishoni mwa juma kwa sababu kufanya hivyo ni kwenda kinyume na utaratibu wa udhibiti.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Desemba 13, 2024 na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Titus Kaguo wakati wa mafunzo ya udhibiti wa huduma za nishati na maji kwa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta).

Kaguo amesema ni muhimu huduma za maji zikakatwa siku za kazi ili mteja aweze kushughulikia tatizo lake na kurejeshewa huduma haraka.

Amesisitiza kuwa kukata maji Ijumaa jioni au Jumamosi na Jumapili ni kwenda kinyume na utaratibu wa udhibiti.

“Hii tabia ya kumkatia mtu maji Ijumaa saa 12 jioni hairuhusiwi kiutaratibu. Mamlaka itakayobainika kufanya hivyo itachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kumfidia mteja gharama alizotumia kupata huduma hiyo,” amesema Kaguo.

Aidha, amewahimiza wananchi kusoma mikataba ya huduma kwa wateja inayotolewa na mamlaka za maji, inaorodhesha haki zao na hatua za kuchukua iwapo haki hizo zitakiukwa.

Kuhusu suala la kubambikiwa bili, Kaguo amekiri tatizo hilo lilikuwepo awali, lakini hatua ya kuweka utaratibu wa mita kusomwa wateja wakiwa nyumbani, imepunguza malalamiko hayo.

“Msomaji wa mita anatakiwa kusoma mita akiwa na mwenyeji ili kila upande ukubaliane na kilichoonekana. Mteja pia hupewa siku tatu za kutoa malalamiko iwapo hakuridhika,” amesema.

Pia, ametoa rai kwa wateja ambao bado wanakumbana na changamoto ya kubambikiwa bili kufikisha malalamiko yao Ewura.

Katibu Mkuu wa Jowuta, Suleiman Msuya, amesema mafunzo hayo yamewawezesha waandishi wa habari kuelewa kazi za Ewura katika sekta za maji, umeme na gesi na kuwahamasisha kutumia kalamu zao kuwaelimisha wananchi kuhusu haki zao kwenye huduma hizi.

Related Posts