Jalada kesi ya kuteka kobe 116 lapitiwa upya

Dar es Salaam. Jalada halisi la kesi ya kuongoza genge la uhalifu na kuteka nyara za Serikali ambazo ni Kobe 116 inayowakabili watu wanane wakiwemo maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) na raia wa Ukraine, limerudishwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwa ajili ya kupitiwa upya.

Hayo yameelezwa leo Desemba 13, 2024 na Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Anna Magutu, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni mfanyabiashara Josephat Moyo (52), mkazi wa Tabata, Deogratius Lugeng’a (40), mfanyabiashara na mkazi wa Kipunguni pamoja na ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania( JWTZ) MT 88046 Sajini  Cosmas Ndomba (39) mkazi wa Kivule.

Wengine ni ofisa wa Jeshi la Wananchi MT 118102 Kassim Abdallah (35) ambaye pia ni  Ofisa Usalama wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ( JNIA) na mkazi wa Tabata Segerea.

Washtakiwa wengine ni Nkanamuli Mgaza (52) ambaye ni ofisa Usalama Uwanja wa Ndege wa JNIA;  Stephano Chedego (51) mkulima na mkazi wa Dodoma;  Mwaluko Mgomole (41) mkulima na mkazi wa Dodoma pamoja na raia wa Ukraine, Olga Kryshtopa (35) mwenye makazi yake Kiev – Ukraine.

Kasala amesema kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa, lakini jalada halisi la kesi hiyo limerudishwa NPS Dodoma ili liweze kupitiwa na kutolewa maamuzi kabla ya kuendelea na hatua nyingine.

Baada ya kueleza hayo, ameomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Magutu baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 30, 2024 kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa saba wapo nje kwa dhamana isipokuwa Kryshtop ambaye ni raia wa Ukraine.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na kumiliki nyara za Serikali.

Katika shtaka la kwanza, ambalo ni kuongoza genge la uhalifu, washtakiwa wanaodaiwa kutenda kosa hilo katika tarehe tofauti, kati ya Januari 2022 hadi Julai 2022, katika Uwanja wa Ndege JNIA uliopo wilaya ya Ilala.

Katika kipindi hicho, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kukusanya, kununua na kusafirisha kobe, kinyume cha sheria.

Shtaka la pili ni kuteka nyara za Serikali, kwa kununua, kukusanya na kuuza kobe 116 wenye thamani ya Sh18, 935, 840 bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori.

Shtaka la tatu ni kumiliki nyara wakidaiwa kwa kwa makusudi kukutwa wakimiliki kobe 116, bila kuwa na kibali cha Serikali.

Related Posts