Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA)imesema watu ambao wanafanya kazi ya kutandaza Waya katika nyumba lakini hawana leseni ya EWURA wajue wanafanya makosa na wakibainika hatua za kisheria dhidi yao zitachukuliwa.
Hayo yameelezwa leo Desemba 13 Jijini Dar es Salaam wakati wa Semina iliyoandaliwa na EWURA kwa ajili ya waaandishi wa habari ambao ni wanachama wa Chama cha Waandishi wa habari Tanzania(JOWUTA) na katika Semina hiyo mada mbalimbali zimetolewa ,lengo likiwa kuwajengea uwezo Waandishi kufahamu majukumu ya mamlaka hiyo.
Akizungumza katika Semina hiyo Kaimu Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki Mhandisi Mwanamkuu Kanizio amesema pamoja na majukumu mengine EWURA inawajibu wa kutoa leseni kwa mafundi umeme wanaofanya kazi ya utandazaji waya katika nyumba kabla ya kuunganishwa na huduma ya umeme wa TANESCO.
“Watu ambao wanafanya kazi ya kutandaza waya katika nyumba halafu hawana hivyo vibali ni kosa kisheria na kanuni inaelekeza kwamba mtu akikutwa anafanya kazi ya utandazaji Waya bila kuwa na kıbali cha EWURA atatozwa faini lakini pia anaweza kuhukumiwa kifungo. Pia anaweza kupata adhabu zote mbili kwa pamoja kutokana na mazingira ya kosa lenyewe.”
Alipoulizwa EWURA inafanya nini ili kuhakikisha jamii inatumia mafundi ambao wanaleseni ,amejibu kwanza wanawaelimisha na wamekuwa wakitoa elimu katika ofisi za kanda mbalimbali kwa kutoka katika Mkoa mmoja hadi mwingine.
Pia wamekuwa wakifanya semina elekezi kwa wanafunzi ambao wako vyuoni kwa kuwajengea uelewa jinsi ya kuomba leseni ili kuwa na mafundi wengi wenye leseni.”EWURA imeunganisha mfumo wetu wa utoaji leseni na Mfumo wa maombi ya huduma ya umeme wa Tanesco inayojulikana kama NI- Connect.
“Takribani miaka miwili nyuma Mtanzania yeyote hawezi kuunganishiwa umeme bila kupitishwa katika mifumo miwili, maana yangu ni nini unapokwenda kuomba umeme TANESCO watakupa orodha ya mafundi walioko katika mifumo hiyo na hapo utapata fundi atakayehusika kutandaza waya za umeme katika nyumba.”
Akieleza zaid amesema kuwa wanafahamu kuwa kuna vishoka au mafundi wenye leseni zao lakini wamekuwa wanafanya udhibiti kama wanavyofanya kwa TANESCO au mtoa huduma yoyote ya umeme.
“Kwahiyo mafundi wenye leseni tumekuwa tunawakagua na katika kaguzi zetu tuliwataka watuoneshe kazi ambazo wamezifanya wao.Wanapoenda kinyume na utaratibu huo kanuni imeelekeza adhabu ikiwemo ya kusitishwa kwa leseni ambazo tumewapatia.Tunatoa leseni,tunauhisha leseni lakini tunayo mamlaka kufuta leseni yeyote.”