Chande: Tafiti zisaidie jamii, siziishie kwenye maktaba

Arusha. Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande amewataka wahitimu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kutumia matokeo ya tafiti walizofanya kusaidia jamii kukabiliana na changamoto mbalimbali walizozibaini.

Chande ametoa wito huo leo Ijumaa, Desemba 13, 2024, katika mahafali ya 26 ya chuo hicho, wahitimu 5,854 wa ngazi za Astashahada, Shahada na Shahada ya Uzamili.

Amesema matokeo ya tafiti zao yasiishie kwenye maktaba au machapisho, bali yahusishe jamii moja kwa moja ili yachochee mabadiliko chanya, kuboresha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kulenga kusaidia uboreshaji wa sera kwa masilahi ya Taifa.

“Shirikisheni jamii matokeo ya tafiti zenu ili yawe chachu ya mabadiliko chanya. Hii itasaidia kuongeza tija katika uchumi, maendeleo ya kijami na kutoa mchango wa kitaalamu katika uundaji wa sera,” amesema Chande.

Aidha, Naibu Waziri huyo amesema mwelekeo wa sasa wa elimu ya juu nchini ni kufanikisha umataifishaji wa elimu.

Amesema dhana hiyo pia inalenga kuhakikisha wahitimu wanapata elimu inayokidhi viwango vya kimataifa na kuwajengea uwezo wa kufanya kazi popote ulimwenguni.

Awali, Mkuu wa chuo hicho  Profesa Eliamani Sedoyeka amebainisha kuwa kati ya wahitimu hao, wanaume ni 3,601 na wanawake 2,253.

Amesema wahitimu hao wametunukiwa shahada na astashahada katika fani mbalimbali, zikiwemo Usalama wa Mtandao, Menejimenti ya Maktaba na Taarifa, Uanagenzi katika Usimamizi wa Utalii na Ukarimu pamoja na Shahada za Uzamili katika Usimamizi wa Elimu.

Profesa Sedoyeka amesema kupitia mradi wa HEET, wanatarajia kuhuisha mitalaa 18 ifikapo mwaka wa masomo 2025/26 ili iendane na mahitaji ya soko la ajira huku ikijumuisha masuala ya elimu jumuishi, jinsia na mabadiliko ya tabianchi.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho, Dk Mwamini Tulli amesema miongoni mwa malengo ya chuo hicho ni kuongeza idadi ya wanafunzi kila mwaka wa masomo.

Amesema wanatarajia kufikia uwezo wa kuchukua wanafunzi kati ya 40,000 hadi 60,000 katika kampasi zote.

Related Posts