KWANINI EWURA WALIAGIZA MITA YA MAJI ISOMWE MMILIKI AKIWEPO? SOMA MAJIBU

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ambayo ni taasisi ya udhibiti wa huduma za nishati na maji inayojitegemea, iliyoundwa kwa Sheria ya EWURA Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania na marekebisho yake Na. 6 ya mwaka 2019 , imeeleza sababu za kwanini ilitoa maagizo kwa mamlaka za maji kusoma mita za maji wakati mmiliki wa mita akiwepo.

Akizungumza leo Desemba 13,2024 Jijini Dar es Salaam Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa EWURA Titus Kaguo wakati akitoa mada katika semina ya Waandishi wa habari ambao ni wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania(JOWUTA) amesema walitoa maagizo hayo baada ya kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji wa maji.

“Niseme tu mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ilishatoa miongozo huko nyuma ambayo inataka usomaji wa mita za maji uwe anasoma mita wakati mtu mwenye mita kwa maana ya mmiliki akiwepo.Sio unasoma mmiliki wa mita hayupo ,anatakiwa mmiliki wa mita awepo katika eneo la mita

“Kwanini EWURA iliagiza hivyo kulikuwa na malalamiko ya kubambikiziwa bili kwa
maana ya kwamba watumishi wa mamlaka mbalimbali wanafika mahala halafu wanakuletea hii ndio bili yako.Sasa tukatoa agizo mita zinaposomwa kwanza mwenye mita awepo.

“Na baada ya kusoma wote wakiwemo utatumwa ujumbe kwenye simu na tunaamini Watanzania wanaupata ule ujumbe ambao unaweza kuwa unakuambia mita tuliyoisoma inasema Kiasi hiki na unatolewa muda wa siku mbili au tatu kwa ajili ya kujadiliana kwamba hii bili iliyoletwa ni halali au si halali…

“Ukishakaa siku tatu bila majibu wanakuletea bili halısı ya kulipa ,kwahiyo baada ya kufanya hivyo tunaona malalamiko yanapungua. Lakini kingine ambacho tuliagiza ni marufuku kwa mamlaka ya maji kukata maji siku za mapumziko kwasababu kuu inakuwa kama unyanyasaji.

“Kama mtu anakuwa na makosa mkatie siku ambayo atakuja ofisini kutatua kosa ili huduma irudi,kwaniyo hii ya kusema mtu anakata siku ya Ijumaa saa 12 jioni hiyo hairuhusiwi kitaratibu na wala hairuhusiwi kiudhibiti na mamlaka inayofanya hivyo itakuwa inakosea na haitakiwi kufanya hivyo sababu inaweza kuchukuliwa sheria ili kuwajibika kwa kile wanachokifanya,”amesema Kaguo.

Hata hivyo amesema Watanzania wanatakiwa kuwa makini na wanawahamasisha wasome mikataba ya huduma kwa wateja kwa mamlaka mbalimbali na kufafanua kuwa mamlaka zilizopo hapa nchini zile mamlaka 25 za mikoa zote zinamikataba ya huduma kwa wateja.

“Ule mkataba wa huduma kwa wateja ,inakupa wajibu wa wewe ufanye nini na wajibu wa mamlaka ifanye nini. Lakini kutokana na mamlaka nyingi hazihamasishi kujulikana kwa mikataba hiyo ili Watanzania hawa wasiibuke na kuanza kudai haki zao.

“Kwahiyo kupitia Chama cha Waandishi wa habari (JOWUTA) tunaomba mtusaidie kufikisha ujumbe kwa Watanzania kwamba kila mamlaka ya maji inamkataba wa huduma kwa wateja.Soma ule mkataba unasema nini ,watu wengi wanashindwa kupata haki kwa kuwa mamlaka za maji hazitangazi mikataba yao ya huduma kwa wateja…

“Kama EWURA ambavyo tumekuwa tunasema mkataba wa huduma unasema nini ili utubane sababu lengo la mkataba wa huduma kwa wateja tunataka utubane sisi tunaotoa huduma.Kwahiyo na sisi tumewapa mikataba ile mamlaka za maji tukazigawa kwa watu lakini watu wa mawasiliano hatusikii wakitangaza mikataba ya huduma kwa wateja.”

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania(JOWUTA)Suleiman Msuya akielezea kuhusu semina hiyo amesema kuwa walitoa ombi kwa EWURA kutoa mafunzo kwa Waandishi wa habari ambao ni wanachama wa JOWUTA zaidi ya 400 waliopo nchini.

“Hivyo elimu hii ambayo imetolewa leo kwa Waandishi wa habari ilikuwa imelenga kuangalia ni namna gani tunakuwa sehemu ya EWURA katika kueleza masuala yanayofanana na kazi ya EWURA ikiwemo mikataba ya huduma kwa wateja

“Haya yote tusingeyajua kama tusingepata mafunzo haya na sisi kama JOWUTA tunawaomba waandishi wa habari kutumia fursa hii kuileza jamii yanayofanywa na EWURA na tuwe na ushirikiano chanya kati yetu na taasisi nyingine zinazofanya kazi na EWURA,”amesema Msuya.

EWURA NI NINI?

Kwa kukumbusha tu Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ni taasisi ya udhibiti wa huduma za nishati na maji inayojitegemea, iliyoundwa kwa Sheria ya EWURA Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania na marekebisho yake Na. 6 ya mwaka 2019.

EWURA, ilianza kazi rasmi Septemba, 2006 ikiwa na wajibu wa kusimamia shughuli zote za kiuchumi na kiufundi katika sekta za Nishati(umeme, petroli na gesi asilia); na Maji (majisafi na usafi wa mazingira).

Katika kutekeleza wajibu wake, kwa uwazi na kwa manufaa ya wote, EWURA inazingatia sheria za kisekta, sera na miongozo ifuatayo:-

Sera ya Taifa ya Nishati (2015), Sera ya Taifa ya Maji (2002), Sheria ya EWURA, Sura Na. 414; Sheria ya Umeme, Sura Na. 131; Sheria ya Petroli, Sura Na. 392; Sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira, Sura Na. 279; kanuni na miongozo mbalimbali.




Related Posts