Yanga yafuata kipa jeshini, ni mrithi wa Metacha

MOJA ya eneo ambalo Yanga itaingiza ingizo jipya msimu ujao ni katika nafasi ya kipa na hesabu zao zimeenda kwa kipa namba moja wa timu ya Jeshi la Magereza, Tanzania Prisons.

Mabosi wa Yanga wanajipanga kuvamia katika klabu hiyo yenye maskani yake mkoani Mbeya ikimfuata kipa namba moja wa kikosi hicho, Yona Amos ambaye msimu huu alikuwa na dakika 90 bora alipowatibulia Simba wakati Tanzania Prisons waliposhinda 2-1 ugenini kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba kipa huyo anapigiwa hesabu kuwa mrithi wa Metacha Mnata ambaye kuna asilimia kubwa kwamba akavaa jezi za timu hiyo mpaka mwisho wa msimu huu kisha ataachwa.

Metacha mkataba wake na Yanga unafikia mwisho wa msimu huu akirejea klabuni hapo kwa mara ya pili lakini kinachoelezwa kumng’oa ni nidhamu yake ambayo haiwavutii mabosi wa klabu hiyo.

Yona akiwa chaguo namba moja pale kwa Wanajeshi wa Magereza amefikisha jumla ya klinshiti sabaa msimu huu.

Yanga hesabu zao inataka nafasi ya Metacha izibwe na kipa mzawa ili aje kusaidiana na kipa wao namba moja Djigui Diarra na Aboutwalib Msheri.

Inaelezwa Diarra ambaye anaongoza kwa klinshiti 13, kwa makipa wa ndani anamkubali sana Yona ambaye kila alipokuwa akikutana naye kwenye ligi amekuwa akizungumza naye mwisho wa mchezo na kumpongeza lakini pia akimjenga ili aje kuwa kipa bora.

Yanga inataka kuiwahi Prisons ambayo inajipanga kumwongeza mkataba kipa huyo haraka ambao unafikia tamati mwisho wa msimu na wanajeshi hao wanataka kabla ya kumalizika kwa msimu wawe wameshakamilisha mchakato huo.

“Yanga bado hawajatufuata kama wanamtaka Yona lakini sisi hesabu zetu tunataka kumwongeza mkataba haraka kijana wetu ikiwezekana kabla ya msimu kumalizika jambo liwe limekamilika,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu wa Prisons, Ajabu Kifukwe.

Kwa upande wake Yona ameliambia Mwanaspoti kuwa ingawa hana kipingamizi cha kwenda kuitumikia Yanga lakini bado hajapokea ofa kutoka kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.

“Mkataba wangu na Prisons unakwisha mwisho wa msimu huu, naheshimu mkataba huu ambao unaelekea mwishoni lakini sote tunafahamu Yanga ni klabu kubwa ambayo kila mchezaji anatamani kuichezea kama watakuja kwa kufuata utaratibu sitakuwa na tatizo ingawa sasa bado hawajanifuata,” alisema Yona.

Related Posts