Mwanza. Watoto wanne wamefariki dunia katika Kijiji cha Isengwa, Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu wakijaribu kuokoana kwenye dimbwi la maji, baada ya mwenzao kuteleza na kutumbukia wakati wakichota maji ya kufua nguo.
Akizungumza kwenye eneo la tukio leo Desemba 13, 2024, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Simiyu, Faustin Mtitu amesema watoto hao ambao ni Neema Ndogo (16), Mery Kibunje (17), Nkwaya Sanga (15) na Lucia Samson (16), wote wamezama Desemba 12, 2024 saa 11 jioni .
“Kwa maelezo tuliyoyapata kwenye eneo la tukio ni kwamba watoto hao wamefika kwenye shimo hilo kwa lengo ya kupata maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kufua nguo na matumizi mengine ya nyumbani.
“Inavyoonekana kwa bahati mbaya wakati wanaendelea kuchota maji hayo, mtoto mmoja wapo aliteleza na kutumbukia kwenye shimo lililokuwa limejaa maji na katika jitihada za kujaribu kuokoana, wenzake nao wakazama na kuzidiwa na maji na hatimaye kupoteza maisha,” amesema Mtitu.
Mtitu amesema matukio ya watoto, watu wazima na hata mifugo kupoteza maisha kwenye madimbwi, mashimo, visima, mabwawa yanaongoza kwa vifo na kuripotiwa mkoani Simiyu, hivyo amewataka wazazi na walezi kuchukua tahadhari.
Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo, Surawati Marieta, shimo lililochukua maisha ya watoto hao, watatu wakiwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lagangabilili, lilichimbwa kwa ajili ya kutoa changarawe na kufyatua matofali.
Amesema Serikali ichukulie mkazo maana eneo hilo lina mashimo mengine mawili yenye kina kirefu, akiomba yafukiwe kwa kuwa yamekuwa kikwazo kwenye jamii yao.
“Tunaiomba jamii ishirikiane kufukia mashimo hayo kwa kuwa yanahatarisha watoto wetu,” amesema.
Shuhuda mwingine aliyejaribu kuwaokoa watoto hao, Njile Shambani amesimulia kuwa: “Mmoja alikuja kuchota maji hapa naona alikanyaga pabaya…mwingine jinsi ya kumuokoa akawa na yeye ameteleza, watatu naye akamuona mwenziye anapiga kelele akamfuata na wanne hivyo hivyo.
“…nikaingia na mlingoti, nikaanza kuwatafuta kwa mlingoti, nikabahatisha kumuopoa mmoja, alikuwa ameshakata moto (fariki), ikabidi nitafute mwingine, nikafanikiwa kumuopoa…wakabaki wawili, ikabidi nizame kuwatafuta humo ndani.”