Wakati kwa sasa watu wakiona kuwa na nyumba ya ghorofa ndio kielelezo cha mafanikio ya kimaisha, watu wengi hawajui kuwa Wasafwa walishakuwa wajanja siku nyingi kwa kuishi sio tu ghorofani, lakini hata kuwa na choo ndani ya nyumba.
Japo hazikuwa ghorofa za zege, iliwatosha watu wa kabila hilo kujenga maghorofa yao na kisha kuezeka kwa nyasi!
Wasafwa ni jamii inayopatikana katika Mkoa wa Mbeya, ambao licha ya zamani kuwa wengi inaonekana wamezidiwa na Wanyakyusa.
Kwa sasa Wasafwa wengi wamesogea pembezoni mwa mkoa huo na kwenda kuishi hasa maeneo ya mlimani.
Hali hiyo imewafanya Wanyakyusa kusikika zaidi kwa kuwa wao ndio wamebaki katikati ya jiji hilo na pia ndio wenye maendeleo ya kimaisha ikiwamo elimu.
Ofisa Elimu wa Kijiji cha Makumbusho, Wilhelmina Joseph, anasema jamii hiyo kiasili ni wafugaji na wakulima.Mazao wanayolima ni pamoja na viazi, mahindi na nafaka nyinginezo.
Katika asili yao kwenye makazi, anasema Wasafwa hujenga nyumba tatu; ya kwanza ni ya baba na mama baada tu ya kuoana ambayo ni nyumba kubwa ya ghorofa.
Ofisa huyo anasema wenza hao wakizaa, baba, anasogea pembeni kwa kujenga nyumba nyingine ya pili na kumuacha mama kwenye nyumba kubwa akiwa na mtoto.
“Katika nyumba hiyo chini kuna sehemu inayotumika kwa kupika, na ndio sebuleni na juu na kwa ajili ya kwenda kulala.
“Ili kupanda ghorofani kuna ngazi ambayo huwekwa usiku na kuondolewa asubuhi. Ngazi hii pia ni mahususi kwa ajili ya kujilinda na adui usiku na pia wanapokuwa juu ni rahisi kumuona adui mapema na kupambana naye,”anafafanua.
Hata hivyo, anasema baada ya baba kujenga nyumba nyingine, hiyo kubwa humuacha mama na mtoto.
Ili usiku wasiende nje wenyewe kujisaidia, kuna shimo limechimbwa ambapo hujisaidia hapo na mama kumwagia majivu ili kusitoe harufu na kunapokucha huzoa na kwenda kutupa kinyesi porini.
Pia sababu ya kujenga na kuishi nyumba pembeni ni kwamba mama baada ya kuzaa hawakutani kimwili ndani ya miaka mitatu na baba.
“Inafanywa hivi kumpa nafasi mama ya kulea na ya kurudisha hali yake ya kawaida baada ya hekaheka ya ujazito. Jingine ni kuepuka kuzaa watoto waliofuatana sana,”anasema Wilhelmina.
Katika nyumba hiyo pia mama ataendelea kuishi hapo na watoto atakaondelea kuwazaa hadi watakapotimiza umri wa kulala wenyewe na kwa wa kiume huanza kulala wenyewe mara baada ya kutimiza miaka kumi. Hawa hulala sehemu ya chini ambapo kuko jiko na sebule.
Wale wa kike wao hulala na mama mpaka pale wanapotimiza miaka 18 au kuolewa.
Mama akikamilisha miaka mitatu ya ulezi wa mtoto, akitaka kukutana na baba, atamfuata kwenye nyumba yake na huko hujifanya kama anampelekea chakula, kumbe lengo ni kutimiza haja ya kindoa pasipo watoto kujua.
Nyumba ya tatu inayojengwa ni kwa ajili ya watoto wa kiume na huhamia huko mara baada ya kufikisha miaka 13.
Watoto hao katika nyumba hiyo wanaishi na mbuzi, ambapo imegawanywa katika sehemu mbili ya kwanza ya kulala watoto hao na ya pili ya kulala mbuzi.
Pia katika umri wa miaka 12 hadi 13, Wilhelmina anasema ndipo watoto hao hufundishwa majukumu ya familia watakaopokuwa baba ikiwa ni pamoja na kuwa wachapakazi,
Jingine wanafundishwa kutunza na kuihudumia familia, wanafundishwa kuwa wajasiri na kuwa walinzi wa familia.
“Yote haya hufundishwa na wazee, au pale wanapokwenda kwenye mila za jando na unyago.Licha ya watu kuzipiga vita hizi mila zina umuhimu na kwa hali ilivyo sasa kuna haja ya kuzirejea, anasema na kuongeza:
“Kwani hata kwa upande wa watoto wa kike nao hufundishwa namna ya kuwa mama bora, kumlea mume, kufundishwa shughuli zote za nyumbani, kufua, kupika na shughuli zingine za nyumbani.
Pia wanafundishwa namna ya kujisafisha, kujisitiri na kushiriki katika shughuli za kijamii kama misiba, sherehe na nyinginezo.
Anasema moja ya faida za mafunzo hayo ya unyago kwa wasichana ni kwamba zamani mtoto akishafundishwa, hakuweza kuwasogelea wanaume, tofauti na sasa ambapo mabinti wanajua mambo kuliko watu wazima.
‘’Utakuta mtoto wa miaka 10, 11 wapo katika uhusiano, ndio hao tunasikia wanalawitiana, wanabakana, wakati zamani watoto walifundishwa ni vibaya kumsogelea mtoto wa kike au wa kiume,’’ anaeleza.