Mambo saba ya kuzingatia ulaji wa sikukuu za Krismasi, mwaka mpya

Dar es Salaam. Baadhi ya wataalamu wa lishe nchini wameshauri mambo saba kuepuka uzito kupitiliza na maradhi yasiyo ya kuambukiza yanayochangiwa na ulaji usio sahihi wakati wa sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.

Mambo hayo ni pamoja na kutokula aina moja ya mlo kwa siku, kuepuka matumizi ya mafuta kwa wingi, kunywa juisi za kutengeneza badala za vinywaji vya viwandani.

Pia kula vyakula kwa mpangilio na kwa kiasi, kutumia kwa uangalifu matunda yenye kiwango kikubwa cha sukari pamoja, kupunguza vyakula vyenye wanga na kula mbogamboga kwa wingi.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Talker Research ya Marekani, mtu mmoja kati ya wanne anaongezeka uzito wa hadi kilo tano msimu huu wa sikukuu.

Taasisi hiyo imesema, watu duniani kote wanaamini mwisho wa mwaka ni mwezi wa mavuno, hivyo kula vyakula vyenye mafuta zaidi kuliko vile walivyokuwa wakila miezi ya nyuma.

Aidha,  kwa mujibu wa utafiti huo pia watu wanapaswa kuzingatia ustawi wao wa kiafya mwaka 2025 kwa kulenga lishe bora, kuongeza mazoezi ya mwili na kuimarisha tabia ya kujitunza.

Akizungumza na Mwananchi  Desemba 13, mtaalamu wa lishe wa Wizara ya Kilimo, Magreth Natai, amesema ni muhimu kuepuka ulaji wa vyakula vyenye mafuta kama chipsi, kwani si salama kwa afya na ni chanzo cha ongezeko la uzito.

Amefafanua uzito unapooongezeka kutokana na wingi wa mafuta mwilini ndio humsababishia mhusika kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo kisukari na presha.

Amesema wakati wa sikukuu ni muhimu kula vyakula visivyokobolewa akishauri matumizi ya unga wa dona, mafuta machache, kutopika mboga za majani sana na kuepuka chumvi nyingi.

“Mfano soseji zina chumvi nyingi, ikiwezekana tupike kiasili kuchemsha baadhi ya vyakula vyetu na kuweka mafuta machache, pia badala ya kutumia vinywaji vya viwandani tutengeneze juisi wenyewe,” amesema.

Magreth ameshauri ulaji wa vyakula ukidhi mahitaji ya mwili na sio kula ilimradi kujaza tumbo,

Amesema mtoto asipokula mlo kamili ukuaji wake wa akili utakuwa duni na mwili hudumaa.

Naye Husna Faraji, mtaalamu wa lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) amesema ni muhimu nyakati zote jamii kuzingatia ulaji wa vyakula mchanganyiko.

“Kipindi hiki cha sikukuu,  vyakula vingi vinavyotumika sio sahihi utakuta ni kundi moja pekee ndio watu hutumia, mfano matumizi mengi ya chumvi, mafuta na vyakula kundi la wanga ni kubwa, hata uandaaji wa vyakula hivi  bado ni mbovu,” amesema.

Amesema wakati wa sikukuu makundi ya vyakula kama mboga za majani, matunda husahaulika na vyakula vya viwandani hushika hatamu, jambo analosisitiza si salama kwa afya.

“Vyakula hivi vya viwandani huongeza uzito na kuleta hatari ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” amesema.

Kwa upande wake, mtafiti wa lishe wa Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) Maria Ngilisho, ameshauri wakati wa msimu wa sikukuu watu kuzingatia ulaji kiasi.

“Vyakula vyenye mafuta mengi na vile vyenye sukari nyingi ni vya kutumia kwa angalizo kubwa, nafaka, mizizi yenye wanga na ndizi za kupika ambavyo hutoa kirutubishi cha wanga navyo ni vya kuliwa kwa kiasi kwani,” amesema.

Amesema hatima ya vyakula hivyo mwilini huishia kuwa sukari, ambayo kuhifadhiwa mwilini katika hali ya mafuta. 

Mbali na vyakula hivyo Maria ameelekeza kundi lingine la chakula la kutumia kwa uangalifu ni matunda. Hii ni kutokana na kile alichosema matunda yana sukari.

“Kuna ongezeko la kasi ya ugonjwa wa kisukari aina ya pili, inashauriwa kula matunda kwa kiasi na sio kula matunda mengi ili upate afya kama ilivyokuwa ikielekezwa siku za nyuma,

“Tunapaswa kula matunda mawili ya aina tofauti kwa siku moja, kwa mfano, ukipata chungwa moja na ndizi mbivu moja,  hayo yanatosheleza kwa mtu mmoja kwa siku moja,” amesema.

Maria anashauri wakati wa sikukuu watu kula kwa mpangilio walau mara tatu kwa siku (asubuhi, mchana na jioni),

“Pia pata asusa mara mbili (katikati ya milo mikuu). Kula kwa mpangilio kunauwezesha mwili kuchakata chakula chote, kukitumia, kukihifadhi, na kupumzika kabla ya kupokea chakula kingine. Hii pia inasaidia sukari kwenye damu iwe katika viwango sahihi,” amesema.

Novemba 12, 2024 Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi juzi alishauri jamii kuzingatia mtindo bora wa maisha, akionya ulaji wa nyama na unywaji pombe kupitiliza.

Mbali ya hayo kupitia mkutano wake na waandishi wa habari akitoa salamu zake za Krismasi kwa jamii, alisema mtu anapojipa muda kati ya mlo mmoja na mwingine anausaidia mwili kujisafisha, hivyo kujiondoa kwenye hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza.

Amesema chakula kina uwezo wa kumuondolea mtu ugonjwa au tatizo alilonalo; vilevile kinaweza kumsukuma mtu kuingia katika magonjwa yasiyoambukiza.

“Mimi sio mganga wa kienyeji wala mchungaji lakini naweza kufanya ugonjwa ukapotea, chakula kinaweza kukuondolea tatizo ulilonalo, nampa mgonjwa maelekezo kuhusu chakula na ugonjwa unatoweka,” amesema.

Naye mkufunzi wa mazoezi, Godyfrey Mkinga, maarufu ‘Denzel Trainer’ amesema wakati wa msimu wa sikukuu,  ni muhimu watu kufanya mazoezi wanapokuwa nyumbani bila kujalii wapo sehemu gani.

“Mara nyingi wakufunzi wengi wa mazoezi katika msimu huu wa likizo bado tunawahimiza wanafunzi kufanya mambo yaliyo mema,

“Nidhamu ya mazoezi iwe palepale ulaji mzuri wa chakula wanafunzi tunawapa malengo kuwa wanapoondoka warudi wamepungia kilo sio kuongezeka,” amesema Denzel.

Amesema ili kukomesha hilo kwa upande wake hulazimika kuingia makubaliano na wanafunzi wake ya kulipa fidia, ikiwa  watarudi  mazoezini wakiwa wameongozeka mwili.

Related Posts