Dar/mikoani. Hatima ya nani atateuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwania nafasi za uenyekiti wa kanda, itajulikana baada ya Kamati Kuu kujifungia kwa siku tatu kuanzia kesho Jumamosi hadi Jumatatu.
Pamoja na wateule hao kujulikana, baada ya kikao hicho, msimamo wa chama hicho kuhusu kauli ya Makamu Mwenyekiti wake Bara, Tundu Lissu juu ya fedha chafu kuvuruga uchaguzi wa ndani unatarajiwa kuwekwa bayana, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ndani ya chama hicho.
Chadema itafanya kikao cha Kamati Kuu, ambacho pamoja na mambo hayo mawili yanayotarajiwa, pia itabeba ajenda za hali ya kisiasa, kufutwa kwa uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti mkoani Njombe, maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa na tathmini ya maandamano yaliyofanyika hivi karibuni.
Kiu ya wengi, nje na ndani ya kamati kuu hiyo ni mrejesho wa chama hicho juu ya kauli ya Lissu ya Mei 2, mwaka huu mkoani Iringa, aliyodai uwepo wa fedha zilizomwagwa kwenye uchaguzi wa ndani wa Chadema.
Katika hotuba yake siku hiyo ambayo imeibua mjadala ndani na nje ya chama, Lissu alisema: “Wakati nakuja hapa Iringa jana na juzi kulikuwa na mtafaruku mkubwa sana, sijui kama mnafahamu, ndani ya chama chetu kuna pesa nyingi ajabu kwenye uchaguzi huu.
“Leo kwenye uchaguzi kuna hela ya ajabu, ninyi mnafikiri hiyo hela ni ya wapi? Mnafikiri hiyo hela ni ya nani? Mnafikiri hiyo hela itatuacha salama? Ukitaka kujua kwamba hatuko salama, fuatilia mitandaoni,” amesema Lissu.
Mjadala wa kauli hiyo ya Lissu imejadiliwa ndani na nje ya Chadema, na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuifuatilia.
Tayari Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamdun alilieleza gazeti hili kuwa taasisi hiyo inafuatilia jambo hilo.
Ndani ya Chadema hakuko shwari juu ya kauli hiyo. Mmoja wa makada wa chama hicho aliliambia gazeti hili: “Kamati kuu ijayo itakuwa moto, suala la Lissu lazima litajadiliwa kwa sababu lina mazingira mengi, hata mkutano wenyewe haukupaswa kufanyika, lakini wao sijui walilazimisha au vipi.”
Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema kamati kuu itakutana kuanzia Mei 11 mwaka huu.
Mrema amesema pamoja na ajenda nyingine, mambo yafuatayo yatafanyika: Kupokea taarifa ya uchaguzi katika ngazi mbalimbali za chama, kupokea taarifa tathmini ya maandamano ya awamu ya kwanza ya mikoa katika wiki na kuweka mwelekeo awamu ya pili ya maandamano.
Ajenda ya tatu itakuwa kufanya usaili na kuteua wagombea wa nafasi za uongozi katika Kanda nne za Nyasa, Serengeti, Victoria na Magharibi ambapo jumla ya wagombea wa nafasi mbalimbali 135 watafanyiwa usaili.
Nafasi zinazowaniwa ngazi ya kanda ni; mwenyekiti, makamu mwenyekiti, mhazini, wenyeviti wa mabaraza ya chama hicho ya vijana (Bavicha), wanawake (Bawacha), wazee (Bazecha) na katibu wa kanda.
Pia umetolewa mwaliko kwa wanachama wote waliochukua fomu za kuwania nafasi hizo katika kanda za Nyasa, Serengeti, Victoria na Magharibi, ukiwataka kuwepo Dar es Salaam kuanzia Mei 11, mwaka huu na kujisajili Makao Makuu ya Chama.
Licha ya Mrema kutokufafanua zaidi, gazeti hili limedokezwa kuwa kikao hicho kitakachofanyika Dar es Salaam, maazimio yake yatatolewa kwa umma na mwenyekiti (Mbowe).”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Aviti Mushi amesema kamati kuu itakayokaa kuanzia kesho itakuwa ya aina yake kulingana na yanayoendelea, hasa kauli ya Lissu iliyoibua mjadala ndani na nje ya Chadema.
“Kamati kuu ndicho chombo kikubwa pia ndani ya Chadema, sasa haya mambo yanayoendelea, hasa tuhuma, mara sijui fedha chafu lazima wayajadili ili kuleta uhai wa chama, sambamba na matukio waliyoyafanya, kutathmini yana mafanikio kiasi gani.
“Lissu ni mwanasheria nguli sana, sidhani kama atatoa maneno asiyokuwa na uhakika nayo au ushahidi, inawezekana kauli alizozitoa zikawa zina ukweli ndani yake na Kamati kuu ijadili na kuzingatia maelezo yake kama ni uchunguzi ufanyike basi,” amesema Dk Mushi.
Dk Mushi pia amezungumzia suala la uchaguzi wa kanda, akisema ni utaratibu mzuri uliowekwa na Chadema wa kuwahoji wagombea wake waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama hicho.
“Ni jambo zuri kuwafanyia usaili wagombea, inawezekana wengine walijaza fomu kwa kujaribu, lazima mgombea atambue anaijuaje nafasi anayoitaka na kwa nini anaona anafaa kuchaguliwa au maendeleo gani atakayoyaleta katika nafasi hiyo,” amesema Dk Mushi.
Uchaguzi wa kanda hizo nne za awali, umekuwa na mvutano, hususan Kanda ya Nyasa ambapo kuna wagombea wawili maarufu wanaochuana – Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu na Mchungaji Peter Msigwa, anayetetea nafasi hiyo kwa muhula wa tatu.
Mvutano baina ya vigogo hao ulikolezwa na kauli ya Lissu, ambaye alikwenda kushiriki maandamano na mkutano wa hadhara mkoani Iringa, ambao vyanzo vya ndani vya chama hicho, na yeye mwenyewe, vinaeleza ni mkutano ambao haukupaswa kufanyika.
“Kamati Kuu ilizuia maandamano na mikutano Kanda ya Nyasa kwa sababu ya joto la uchaguzi. Walifikia uamuzi huo kwa kuona kama yakifanyika yanaweza kuleta mpasuko. Sasa sijajua Lissu kwa nini alikwenda na hili limeleta shida sana,” alisema mmoja wa makada wa Chadema.
“Amekwenda kimakosa, ameongea hayo ya fedha chafu, chama kinatukanwa, yeye mwenyewe kwa nafasi yake ni mwenyekiti wa kamati ya maadili, hafu anakwenda kutoa tuhuma huko nje, yaani ni shida sana.”
Hata hivyo, Lissu mara kadhaa ametetea kauli yake akieleza kwa nafasi yake haoni shida kukemea rushwa hadharani na kuwa hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa akikemea vitendo hivyo.
Mivutano iliyopo imeibua wasiwasi, wa baadhi ya makada wakisema hawana uhakika iwapo watashiriki uchaguzi huo, kama alivyoeleza Rehema Chamila, kuwa pamoja na ukereketwa wake, haoni tena sababu ya kushiriki uchaguzi huo kwa kuwa unaingiliwa na mambo mengi.
“Kwa sasa sioni sababu ya kuumiza akili kufikiria uchaguzi, hizi siasa zina mambo mengi, muda mwingine watu wanajichagua tu,” amesema.
Hoja kama hiyo iliibuliwa na mwanachama mwingine, Hugo Kimaryo aliyesema ni mbinu inayotumika na wagombea na ni wajibu wa mamlaka kufuatilia na kuhakikisha inaidhibiti.
Licha ya hayo, kumekuwa na madai ya Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), kumuunga mkono Joseph Mbilinyi katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Kanda ya Nyasa, huku wanawake (Bawacha) wakihusishwa na Peter Msigwa.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bavicha mkoani Mbeya, Elisha Chonya alilipinga hilo, akisema hawakuwahi kukaa kikao kulijadili hilo na kwamba kila mmoja anampenda mgombea wake kwa utashi wake.
Mwenyekiti wa Bawacha mkoani humo, Elizabeth Mwakimomo naye alikanusha uvumi huo, akisema hata walioonekana kwenda kumchukulia fomu, haikuwa kwa niaba ya baraza hilo.