Mdahalo Uenyekiti  Tume ya Umoja wa Afrika moto

Addis Ababa. Kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) kilifikia kilele Ijumaa wakati Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga alipopanda jukwaani kwenye mdahalo kujadili maono yake kwa bara hilo pamoja na wagombea wengine wawili.

Katika mdahalo huo uliopewa jina la “Mjadala Afrika”, Odinga alikabiliana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahmoud Ali Youssouf na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Richard James Randriamandrato.

Mdahalo huo uliofanyika mjini Addis Ababa na kuonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni kati ya saa 1 mchana na saa 3 usiku, uligusa kwa mapana utangamano wa kiuchumi, amani na usalama, nafasi ya bara la Afrika katika uchumi wa dunia, na kuleta mageuzi katika Umoja wa Afrika (AU).

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Mauritius, Anil Kumarsingh Gayan, alijiondoa mapema mwezi huu. Shindano hilo bado ni la wanaume pekee, maana yake naibu mwenyekiti ajaye ni mwanamke (sheria za AU zinakataza jinsi moja kumiliki uenyekiti na naibu kwa wakati mmoja).

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Odinga alisema: “Katika wakati huu muhimu, ambapo fursa zetu nyingi ziko hatarini kufunikwa na changamoto zinazoikabili dunia, tunahitaji Tume ya Umoja wa Afrika ambayo inaweza kutimiza vipaumbele vya watu wa Afrika – kwa kuchochea utoaji wa huduma na kwa ushawishi wa kimataifa wa bara letu.”

“Ninaamini ninachokihitaji kutufikisha pale ambapo tungependa kuwa katika nyanja ya elimu, afya, uongezaji thamani na biashara. Ninawaahidi Waafrika kwamba nitawaongoza kutoka mbele ili kuhakikisha kwamba tunafikia maono ya waasisi wetu.  Ninasimama hapa kama Mwanamajumui wa Afrika (Pan-Africanist)…Afrika imekombolewa lakini bado kuna kazi ya kufanya na ninaamini kwamba nina kile kinachotupeleka pale tunapotaka kuwa,” aliongeza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahmoud Ali Youssouf kwa upande wake, alisema ana nia ya kubadilisha ufadhili wa Afrika na kufanya kila awezalo kuhakikisha kuwa Umoja wa Afrika una vyanzo vyake vya mapato.

“Pia, nitakuza biashara ya ndani ya Afrika, ambayo inapaswa kwenda zaidi ya asilimia 80. Na nitaondoa vizuizi vyote visivyo vya kikodi na kuwezesha usafirishaji huru wa bidhaa na watu katika bara zima,” amesema.

Iwapo atachaguliwa, mwanadiplomasia huyo aliongeza, atahakikisha kuwa bara la Afrika litang’ara katika ulingo wa kimataifa.

“Kwa nadharia, biashara inaweza kuwa chanzo cha mabadiliko ya kiuchumi,” amesema, akibainisha kuwa biashara ya ndani ya Afrika kwa sasa iko katika asilimia 12.6, chini sana ya viwango vinavyoonekana katika kanda kama Ulaya na Marekani.

Amesisitiza uwezo wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), kutetea biashara kama njia ya kuongeza ufanisi wa uchumi wa bara hilo mara tatu.

Kutokana na uzoefu wake binafsi kama mkulima mdogo, amesisitiza maendeleo vijijini na haja ya kuwawezesha wanawake na vijana katika soko la bara.

Wakati uenyekiti wa AU ukionekana kama jukumu muhimu katika kuchagiza mustakabali wa Afrika, wagombea walieleza kupigania masuala muhimu, ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa kikanda, maendeleo ya kiuchumi na mwitikio wa taasisi hiyo katika kukabiliana na migogoro katika bara zima.

Majukumu ni makubwa kwani mshindi hataongoza tu chombo hicho kinazozikutanisha serikali barani Afrika, bali pia atapanga ajenda katika kushughulikia baadhi ya changamoto kuu za bara hilo.

Odinga aliwasili Addis Ababa, Ethiopia, Jumatano kabla ya mdahalo wa moja kwa moja wa Ijumaa ambapo wagombea wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika walielezea maono na ajenda zao.

Waziri Mkuu huyo wa zamani, akitumia muda wake kama Mwakilishi Mkuu wa AU kwa Maendeleo ya Miundombinu, aliangazia vikwazo vya kimuundo vinavyozuia biashara.

“Biashara baina ya Afrika leo hii inasimama kwa karibu asilimia 15,” amesema.

Amebainisha vikwazo visivyo vya kikodi, kutofautiana kwa viwango na miundombinu duni kama vikwazo vikubwa. Akielezea jambo hilo, alidokeza kuwa ilichukua miezi mitatu kwa chai ya Kenya kufika Ghana kutokana na uhaba wa vifaa.

Odinga amependekeza kuongezwa kwa thamani kwa malighafi za Afrika, mfumo wa fedha wa kimataifa uliofanyiwa marekebisho upya, na miradi mikubwa ya miundombinu kama vile reli inayounganisha bara zima ili kukuza ushirikiano na kibiashara.

Youssouf alitetea kuwepo kwa mkakati wa pamoja wa kuimarisha utajiri wa asili wa Afrika.

“Bara letu lina rasilimali nyingi, lakini hazijasambazwa sawasawa au kusimamiwa ipasavyo,” alisema.

Mgombea wa Djibouti alipendekeza kuanzishwa kwa vituo vya kikanda vya ubora ili kuendesha uvumbuzi na utafiti, pamoja na makubaliano ya biashara ya kikanda yenye nguvu ili kupunguza tofauti.

Youssouf pia alizungumzia kuhusu uendelevu, akipendekeza kuwa sera za AfCFTA lazima ziwiane na ulinzi wa mazingira na malengo ya kustahimili hali ya hewa.

Kwa kushiriki katika mdahalo huo, wagombea hao watatu walihutubia umma moja kwa moja kwa mara ya kwanza katika jukwaa la pamoja kabla ya uchaguzi utakaofanyika Februari 2025 baada ya miezi kadhaa ya diplomasia.

Related Posts