Ugonjwa wa migomba wawaliza wakulima wa ndizi Moshi

Moshi. Ugonjwa wa fungashada wa migomba umeleta kilio kipya kwa wananchi wanaolima na kutegemea kilimo cha ndizi, kwa ajili ya chakula na biashara katika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Ugonjwa huo unaosababishwa na kirusi aina ya ‘Fungashada’ kwa kitaalamu unajulikana kama ‘Banana Bunchy top Disease’, huenezwa na vidukari wa migomba wanaopatikana eneo la shingo ya mgomba.

Hata hivyo, ugonjwa huo bado hauna kinga wala tiba ya kemikali yoyote na umekuwa tishio kwa wakulima wa zao hilo nchini, kutokana na uwezo wake wa kushambulia na kusababisha hasara ya zaidi ya asilimia 90 hadi 100 ya uzalishaji wa ndizi kwa msimu mmoja.

Akizungumzia ugonjwa huo, leo Desemba 14, 2024, mtafiti kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu ya Tanzania (TPHPA), Hamadi Lyimo amesema ugonjwa huo uligundulika nchini mwaka 2020 katika Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, kando ya Ziwa Tanganyika na kuathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa zao la ndizi.

Amesema ugonjwa huo ulianza kuonekana katika kisiwa cha Pacific Kusini, nchini Misri mwaka 1900 na baadaye kuenea Sri Lanka na Australia mwaka 1913 kabla ya kuenea nchi za Afrika Mashariki kupitia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), mwaka 1960 na baadaye Burundi kisha Tanzania.

Amesema kwa Tanzania, mikoa saba imeathiriwa na ugonjwa huo ikiwemo Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Mbeya, Kilimanjaro, Kigoma na Mwanza.

“Ugonjwa huu bado tunahangaika kusaka kinga na tiba, lakini hofu kubwa iko katika Mkoa wa Kilimanjaro ambao watu wake wengi wanategemea kilimo hiki kwa chakula na biashara,” amesema na kuongeza:

“Tiba pekee hadi sasa ni kung’oa na kuangamiza migomba inayoonekana kuathirika na kusubiri kwa miezi angalau mitatu kwa ajili ya kuanza kupanda tena migomba mipya tena yenye uhakika na usalama iliyothibitishwa na wataalamu wetu,” amesema.

Migomba iliyoshambuliwa na ugonjwa wa fungashada.

Akizungumza ndani ya mashamba ya wakulima walioathiriwa na ugonjwa huo mjini Moshi, mtaalamu wa magonjwa ya mimea kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Tropiki (IITA), George Mahuku, amesema kwa sasa wanafanya kazi ya kuongeza uelewa miongoni mwa wakulima nchi nzima, ikiwemo namna ya kukabiliana nao na mbinu za kilimo za kupunguza kuenea kwa ugonjwa huo.

“Hatujaona kinga dhidi ya ugonjwa huu, njia pekee zilizotumika na nchi zingine ni kuangamiza kama ilivyo kwa magonjwa mengine ya virusi, hazina kinga za matumizi ya dawa za kuulia wadudu au viuatilifu,” amesema.

Ameeleza kwamba ugonjwa huu wa ndizi umesambaa kupitia upandaji wa mimea ya ndizi kutoka maeneo yaliyoathiriwa na pia huenezwa na wadudu wadogo wa kunyonya majimaji maarufu kama ‘aphids’.

Ofisa Kilimo wa kata za Ng’ambo na Msalanga za Wilaya ya Moshi, Sufiani Mganga amesema kabla ya ugonjwa huo kuibuka, mashamba katika kila kata yalikuwa yakizalisha zaidi ya tani sita za ndizi kwa mwaka, lakini sasa uzalishaji ni chini ya nusu ya tani moja.

“Hii pia inaeleza kwa nini bei ya ndizi imepanda, jambo ambalo linashangaza na kuwavunja moyo watumiaji,” ameongeza Mganga akionya kwamba janga hilo linaweza kusababisha upungufu mkubwa wa chakula siku za mbele.

Ofisa kilimo huyo amesema changamoto kubwa kwa sasa ni kuwashawishi wakulima kuvuna ndizi zao na kuharibu mashamba hasa yaliyoko jirani na yaliyoshambuliwa, kwani wanazitegemea kwa chakula na kipato, lakini kadri wanavyochelewa ndivyo hali inavyozidi kuwa mbaya.

Mkulima wa Mtaa wa Mnazi mmoja, kata Ng’ambo, Allen William amesema kuwa katika shamba lake lenye ukubwa wa ekari 1.5 aliweza kuvuna hadi mikungu 2,000 – 2,500 kwa mwaka na kuuza kwa mkungu mmoja kati ya 15,000 hadi 25,000 kulingana na ukubwa.

“Shamba hili pekee nililolikuta kutoka kwa wazazi wangu ndio limenisaidia kujenga nyumba, kununua maeneo mengine na pia kuhudumia familia ikiwemo chakula na kusomesha, lakini leo ugonjwa huu umekuja hata mikungu miwili natafuta,” amesema na kuongeza;

“Kwa sasa imenisababisha niingie kwenye vibarua kusaka riziki na kulisha familia yangu huku nikisubiri msimu wa kilimo nivune mazao katika mashamba mengine ambayo nilifanikiwa kununua awali,” amesema.

Kwa upande wake, Gabriel Ruben ameiomba Serikali kuongeza nguvu katika utafiti wa ugonjwa huo ili ipatikane kinga na sumu ya kumuua mdudu huyo haraka.

“Ugonjwa huu umetupa hasara kubwa sana na unatishia ustawi wa familia zetu hasa baada ya kutakiwa tuangamize migomba yetu yote ambayo imedumu tangu enzi za mababu ikisaidia mahitaji mbalimbali, kikubwa Serikali iendelee kufanya tafiti wa sumu ya kuangamiza mdudu huyu,” amesema.

Related Posts