Changamoto, fursa za demokrasia kujadiliwa kumbukizi ya Maalim Seif

Dar es Salaam. Kauli mbiu ya ‘demokrasia, uchumi wa soko huru, ajira, changamoto na fursa’ ni miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kujadiliwa katika maadhimisho ya miaka minne ya kifo cha aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Hii ni mara ya nne maadhimisho hayo yanafanyika, tangu kufariki kwa Maalim Seif aliyewahi mwenyekiti wa ACT- Wazalendo na mshauri wa chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar.

Maalim Seif aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CUF, alifariki dunia Februari 17, 2021 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Maadhimisho hayo yatakayofanyika kesho Jumapili Desemba 15, 2024 mjini Unguja yameandaliwa na Taasisi ya Maalim Seif Foundation, ikishirikiana na Taasisi ya Friedrich Naumann, ambapo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud atakuwa mgeni rasmi.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo Jumamosi Desemba 14, 2024, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Maalim Seif, Ismail Jussa, amesema  kauli mbiu hizo zimechaguliwa baada ya tafakuri ya kina ya changamoto zinazoikabili demokrasia na uchumi wa ushindani wa soko duniani kote.

Jussa amesema kumeshuhudiwa kuongezeka kwa tawala za kikandamizaji na ushawishi wa harakati zinazojiegemeza kwenye kutaka umaarufu kama ilivyo kwenye sehemu nyingine za dunia.

Amesema matatizo ya kiuchumi, ukosefu wa ajira na kushuka kwa hali za maisha ya watu kunaathiri mitazamo yao kuhusu demokrasia na kusukuma ongezeko la hali ya kutojali ndani ya eneo la Afrika Mashariki.

“Mkutano huu utawaleta pamoja washiriki 150 wakiwemo wanasiasa, watu wenye ushawishi katika jamii, wawakilishi kutoka asasi za kiraia, waandishi wa habari,wasomi na vijana kwa lengo la kutafakari changamoto hizo.

” Pia tutathmini nafasi ya demokrasia na uchumi wa ushindani wa soko huru katika kuchechemua ukuaji wa uchumi utakaozalisha ajira hasa kwa vijana, ambao idadi yao inaunda asilimia kubwa  ya watu wa Zanzibar, Tanzania na Afrika kwa jumla,” amesema Jussa.

Mbali na mkutano huo, kongamano hilo litatumika  kuzindua kitabu kilichopewa jina la ‘ahadi Iliyotimizwa’ ambacho kimekusanya mashairi 35 yaliyoandikwa na malenga 19 kueleza hisia zao wakati wa msiba wa kuondokewa na Maalim Seif.

Kwa mujibu wa Jussa, katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Utafiti wa Taasisi ya Brenthurst Foundation yenye makao makuu yake nchini Afrika Kusini, Ray Hartley ambaye ni mwandishi wa vitabu vingi kuhusiana na masuala ya demokrasia na uchumi, atatoa hotuba maalumu.

Related Posts