Ibenge afunguka dili la kutua Simba, naachaje…!

Kocha Mkuu wa Al Hilal ya Sudan, Florent Ibenge amesema itakuwa ni heshima kwake endapo atapata nafasi ya kuinoa timu mojawapo za Ligi Kuu Tanzania haswa Simba yenye nafasi ya kuwania mataji na kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baada ya uwepo wa tetesi za Simba kuhitaji huduma yake ili kuziba pengo la aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha, ndipo Mwanaspoti lilipofanya nae mahojiano na kuweka wazi dili hilo.

Ibenge ambaye ni maarufu kwa mashabiki wa Tanzania, alisema bado ana mkataba wa mwaka mmoja na waajiri wake Al Hilal lakini ikitokea nafasi ya kufundisha Tanzania itakuwa ni heshima kubwa kwake.

Siyo mara ya kwanza Ibenge kutajwa Simba kwani tangu alipokuwa akiinoa AS Vita, viongozi wa Wanamsimbazi walionyesha hamu ya kuhitaji huduma yake ingawa mara zote kikwazo kimekuwa kikitajwa kuwa ni mshahara mkubwa ambao hauendani na uhalisi wa uchumi wa klabu za Tanzania.

“Nimeshafundisha nchi nyingi kwa mafanikio nafikiri ikitokea nikapata nafasi ya kuja kufundusha Tanzania itakuwa ni heshima kwangu na naamini pia nitakuwa na muendelezo mzuri kwenye CV yangu,” alisema Ibenge ambaye analijua vyema soka la Tanzania na huenda klabu yake ya Al Hilal ikacheza Ligi hiyo msimu ujao kama sehemu ya kujiweka fiti.

Alipoulizwa juu ya mwenendo wa Simba kwa sasa anauonaje, Ibenge alijibu kwamba: “Sijapata muda mrefu wa kuitazama Simba lakini nilipata wasaa wa kutazama baadhi ya mechi zao kipindi nipo Tanzania na timu yangu kwenye michezo ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Baadhi ya mechi nilizozitazama ni zile za Ligi ya Mabingwa walizocheza dhidi ya Asec Mimosas, Jwaneng Galaxy, hata ile ya Wydad na baadhi ya mechi za Ligi hata zile walizocheza na watani zao Yanga.”

Ibenge anaamini kila kitu kilibadilika baada ya ujio wa Kocha Benchikha huku akishangazwa kuona Jean Baleke akiondoka kikosini hapo na kwenda kucheza Ligi ya Libya.

“Baleke ni straika ambaye alikuwa anafanya vizuri na hakuna kocha ambaye anaweza akamuacha mchezaji anayeleta faida kwenye timu yake, ila kwa sababu sikuwepo ndani ya kikosi siwezi kujua kwa nini mchezaji huyo aliachwa kirahisi,” alisema na kuongeza;

“Ndio maana nimesema kila kocha anakuwa na mipango yake, Simba chini ya Benchikha huenda haikuhitaji mchezaji wa aina yake ndio maana anacheza Libya na sio Tanzania kwenye Ligi ambayo tayari alikuwa ameshaizoea na kufunga pia, naamini haukuwa wakati sahihi wa Baleke kuondoka Simba.”

Akizungumzia timu yake kuja kucheza Tanzania kutokana na machafuko yaliyopo nchini Sudan alisema itakuwa nzuri kwao kwasababu wana nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao, hivyo watakuwa timamu kwa kucheza kwani ilikuwa ngumu kwao kuendelea na ligi wakati familia za baadhi ya wachezaji wapo kwenye hali ngumu ya mapigano.

“Kuja kwetu Tanzania itatusaidia sisi kupata nafasi ya kucheza na kujiweka kwenye hali nzuri ya ushindani kwasababu msimu ujao tunacheza michuano ya kimataifa, hata msimu huu hatukuweza kufanya vizuri sana kwenye mashindano ya kimataifa kwasababu hatukupata muda wa kucheza Ligi, naamini kama tukija Tanzania kucheza kama inavyoelezwa itatusaidia sana na tutafanya vizuri mashinmdano hayo,” alisema Ibenge mwenye umri wa miaka 62.

Ibenge anatajwa kuhitajika na Klabu ya Simba kuwa kocha mkuu wa timu hiyo baada ya kuondoka kwa  Benchikha ambapo kwa sasa ipo na makocha wa muda Juma Mgunda na Selemani Matola ambao hadi sasa wamekiongoza kikosi hicho katika mechi nne, ikishinda tatu dhidi ya Mtibwa, Tabora United na Azam FC huku ikitoa sare dhidi ya Namungo.

Related Posts