Dar es Salaam. Mwezi Desemba una sikukuu nyingi. Sehemu kubwa ya dunia inajiandaa kumpokea Masihi, lakini pia kufunga mwaka tayari kwa kuupokea mwaka mpya.
Kila jamii inausherehekea mwezi huu muhimu kwa utamaduni wake. Wachagga wataenda kulamba kisusio, Waskotish watavaa sketi za drafti, Warusi watakunywa Vodka, na wengine watafululiza kwenye klabu za starehe.
Msimu huu unaungana na likizo za mwisho wa mwaka. Watu wa imani huutumia zaidi wakati huu kutembelea wagonjwa na wahitaji, kuwaombea na kuwapelekea zawadi.
Ni mwezi wa kutakiana heri na kuombeana mema. Kiujumla sehemu kubwa ya watu huuchukulia mwezi huu kama mwanzo wa mwisho wa mwaka, hivyo huitumia zaidi katika kubadilishana zawadi.
Kinyume chake vijana wa kisasa wanaichukulia siku hii kama siku ya kufanya madudu. Wengine watajikusanya katika vikundi kwenda kupiga kelele mitaani.
Fujo za magari na fedha, kuchukuliana mabibi na ufuska hufanywa hadharani. Cha kusikitisha baadhi wanashiriki ngono zembe kiholela, jambo linaloweza kuwaweka kwenye hatari ya maambukizi ya VVU.
Mara nyingi tunaona vijana wakibeba maredio makubwa au wakifungulia muziki wa kwenye gari kwa sauti kubwa.
Wakizurura na machupa ya pombe, au hata misokoto ya bangi na kete za dawa za kulevya. Hali huwa mbaya hasa pale watoto wanapoiga kwa kudhani kuwa hiyo ni namna mpya ya kufurahi. Nao watatafuta uchochoro na kuyarudia madudu kama hayo, wakajiweka kwenye hatari ya kuuvaa uraibu wa shisha.
Namkumbuka mzee wetu wa Kichaga ambaye hakujua sikukuu yoyote zaidi ya Krismasi. Alioa na kuzaa ughaibuni kabla ya kurudi nchini akiiacha familia yake ikiendelea na maisha huko. Wengine wanasema aliipenda asili yake kiasi cha kutoshawishika kubadili uraia na kubaki ugenini.
Aliishi na wafanyakazi wa ndani tu, lakini kila Krismasi aliwakusanya watoto na majirani kufurahi pamoja naye.
Usiku wa kuamkia Krismasi, mzee alikuwa na kawaida ya kukesha sebuleni kwake akiwa na vitabu vitakatifu, mikanda ya video iliyoigizwa kuzaliwa kwa Kristo na majarida mbalimbali yanayohusu siku hiyo.
Angekesha akiimba nyimbo kufuatilizia santuri za akina Jim Reeves, Boney M na kadhalika. Wasaidizi wake walipomkumbusha kuwa ni muda wake wa kulala, aliwajibu
“Hapi Krismas!” halafu akaendelea pale alipoacha kuimba.
Asubuhi ya Krismasi alijikuta palepale sebuleni.
Lakini wasaidizi kwa jinsi walivyomwelewa walikuwa tayari wameshapangiana majukumu ya siku hii muhimu sana kwake.
Walishamuandalia supu ya mkia wa kondoo mezani, wakakata saladi ya matango, karoti na vikorombwezo vingine. Vyakula vinono kwa ajili ya wageni viliandaliwa, na muda ulipofika wote walijumuika mezani huku watoto wakijisosomoa majamvini.
Baada ya chakula ilikuwa sherehe kamili kwa watoto kucheza muziki na wazee kugongeana glasi. Zawadi zilitolewa kwa watoto walioonesha ufundi wa kucheza.
Mida ya jioni wakaachwa wazee waendelee na mvinyo wakati kila mtoto akiondoka na zawadi za lawalawa, sharubati, biskuti na vingine vya kumpelekea mama nyumbani.
Aisee mzee huyu aliandika kumbukumbu inayobaki mtaani kwetu. Somo kubwa alilonifunza mzee ni kusherehekea sikukuu kwa amani pamoja na wenzetu. Inapendeza zaidi kuwa nyumbani na familia, ndugu jamaa, marafiki na majirani.
Aidha uwe mwenyeji au mualikwa, ni vema kuwamo kwenye sehemu ya jamii mkibadilishana mawazo na kuyajenga mapya katika wakati unaokuja. Penye wengi hapaharibiki jambo, unaweza kupata faida ya kutatua matatizo yanayokusumbua kwa muda mrefu.
Sherehe ni siku kama siku zingine. Usikubali kufanya matumizi makubwa yakakwamisha maendeleo yako. Tena furaha yako isiwakwaze wengine, maana fujo kama hizo za vijana huwaathiri wengi. Wao huona kuwa hiyo ni namna ya kujiachia mitaani na kwenye makazi ya watu, lakini ukweli wanasababisha usumbufu kwenye jamii, kuwaathiri zaidi wazee, watoto na wagonjwa wasio na utetezi.
Kama huwezi kujizuia kujiachia basi tafuta maeneo rasmi ya kufanya hivyo. Pengine mwenzetu bila pombe na muziki mnene unakuwa haujakidhi matamanio yako basi nenda baa, klabu za usiku au kwenye viwanja vya dansi na disko. Huko utapiga kelele hadi mwisho wa sauti bila kusumbua watu wengine. Lakini napo kuna masharti yake, kwa mfano huruhusiwi kufanya fujo au kuvunja chupa.
Mwezi huu ukipangiliwa vizuri basi unaleta maana kubwa zaidi hasa unapozingatia upendo kwa wote. Ni vema kujitoa kwa wengine bila kujali tofauti zetu. Inaweza kutokea kutokuelewana kwenye familia juu ya aina ya chakula, vinywaji, mavazi, chaneli ya TV ya kutazamwa na kadhalika.
ikumbukwe kuwa dunia haitaki ubinafsi na ndio maana tuna ndugu, marafiki na majirani. Kila mmoja akiridhika na machaguo ya wenzake, mambo yanakuwa mazuri.
Usisahau kwamba baada ya Krismasi huja Mwaka Mpya. Jitayarishe pia kufurahi kwa mtindo huo wa amani huku ukizingatia ujio wa mwezi Januari.
Jiwekee akiba na kamwe usiruhusu kuteseka na misongo ya ada za watoto, kodi ya nyumba na mahitaji mengine ya lazima ati kwa sababu umejimaliza kwa sikukuu. Kwa maneno haya, nawatakia maandalizi mema ya sikukuu za mwisho wa mwaka na mapokezi ya mwaka mpya wa 2025.