Fountain Gate iko hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa beki na nahodha wa Coastal Union, Jackson Shiga ili kuongeza makali ya safu ya ulinzi, ikiwa ni pendekezo la kocha mkuu, Mohamed Muya.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo, zinasema kocha Muya hajaridhishwa na safu ya ulinzi ya kikosi hicho hadi sasa, licha ya eneo la ushambuliaji kuonekana kumpa matumaini makubwa msimu huu.
“Shiga ni beki mzuri ambaye tulianza kumfuatilia kwa muda mrefu na baada ya kuona ameshindwa kufikia makubaliano na timu aliyokuwepo tukaona ni vyema kuanza mawasiliano naye, japo bado hatujafikia muafaka juu ya hilo,” kilisema chanzo chetu.
Akizungumzia suala hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate, Kidawawa Tabitha alisema huu ni muda wa kila mmoja wao kuzungumza jambo lolote linalohusu usajili kwa sababu wakati wake umekaribia, ingawa wataweka wazi watakapokamilisha.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua kocha Muya amewasilisha ripoti yake kwa viongozi na mojawapo ya maeneo anayohitaji kuongezewa nguvu ni beki wa kati, kutokana na kutokuwa na safu bora ya ulinzi.
Katika michezo 13 iliyocheza kikosi hicho kinachoongozwa na kinara wa ufungaji, Seleman Mwalimu mwenye mabao sita, ni timu ya kwanza msimu huu kwa kuruhusu mabao mengi ikifanya hivyo mara 23, ikifuatiwa na KenGold iliyoruhusu kufungwa 22.
Licha ya hayo, ila Mwanaspoti linatambua pia Shiga ni miongoni mwa wachezaji wanaohitajika na Pamba Jiji, japo viongozi wa timu hiyo mara kadhaa wameonyesha hawana uhitaji wa beki huyo katika dirisha hili linalofunguliwa rasmi kuanzia leo.