Mapilato wa Simba, Yanga CAF hawa hapa

YANGA inatarajiwa kushuka uwanjani jioni ya leo ikiwa ugenini DR Congo kuumana na TP Mazembe, huku Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likiwapangia mwamuzi kutoka Benin, Djindo Louis Houngnandande kulihukumu, huku refa kutoka Madagascar, Andoftra Revolla Rakotojuana amepewa ya Simba na CS Sfaxien.

Yanga na Mazembe zinavaana katika pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika zikiwa Kundi A, wakati Simba na CS Sfaxien ya Tunisia zitaumana Kwa Mkapa katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Tuanze na pambano la Lubumbashi, mwamuzi aliyeachiwa msala wa mchezo huo wa Yanga na Mazembe hii itakuwa ni mechi ya pili kwake katika Ligi ya Mabingwa , kwani Novemba 26, alichezesha pambano kati ya Pyramids ya Misri na GD Sagrada Esperança ya Angola uliopigwa Cairo na wenyeji Pyramids kushinda 5-1.

Katika mechi hiyo, Houngnandande alitoa kadi za njano tatu kadhalika alishawhi kutumika kama mwamuzi wa kati katika mechi tatu za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambapo alitoa kadi 14 za njano, hivyo kufanya awe ametoa jumla ya kadi 17 katika mechi hizo za CAF.

Kwa upande wa Simba na Sfaxien, mwamuzi kutoka Madagascar Andoftra Revolla Rakotojuana ndiye atakayepuliza kipyenga katika mechi hiyo itakayopigwa kesho Jumapili, refa huyo aliwahi kuichezesha Yanga na Al Merreikh ya Sudan katika mechi ya raundi ya pili ya LIgi ya Mabingwa msimu uliopita iliyopigwa Septemba 16, 2023.

Katika mchezo huo, Yanga walishinda 2-0, ambapo mabao yalifungwa na Kennedy Musonda na Clement Mzize, huku mwamuzi huyo akitoka kadi mbili pekee za njano.

Rakotojuana, ambaye anajulikana kwa kutoa kadi nyingi, ana wastani wa kutoa takriban kadi nne kwa mchezo mmoja.

Hata hivyo, kwa michezo yake ya hivi karibuni, mechi ya Yanga dhidi ya Al Merreikh ilikuwa moja ya zile alizotoa kadi chache zaidi.

Katika michezo 10 ya mwisho aliyochezesha, Rakotojuana amekuwa na mwelekeo wa kutoa kadi nyingi, pia ameonyesha kuwa na uwezo wa kutoa maamuzi magumu, kama alivyofanya katika mchezo wa Agosti 25 mwaka huu kati ya Al Hilal Omdurman na Al Ahli Benghazi, ambapo alitoa kadi saba (2 kwa wenyeji na 5 kwa wageni) katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kama ilivyo kwa mechi nyingi alizochezesha, Rakotojuana amekuwa na tabia ya kuwa na matokeo mazuri kwa wenyeji, kwani katika michezo 10 aliyochezesha, wenyeji walishinda mara tano na kupata sare tatu.

Kwa mchezo wa Simba dhidi ya CS Sfaxien, Rakotojuana atasaidiwa na Dembiniana Andreatianarevelo na Pierre Jean Eric Andrevouvouange, huku Pan Amsy Tsimanohitsy atakayekuwa mezani na wote wanatoka Madagascar.

Related Posts