Kocha awaka, kisa kipa wa Azam

KOCHA wa Tabora United, Mkongomani Anicet Kiazayidi amewaka na kusema ushindi iliyoupata timu hiyo juzi dhidi ya Azam FC, haukutokana na makosa ya kipa wa Wanalambalamba kama inavyosemwa na mashabiki na wapenzi wa soka, ila ni ubora wa kikosi alichonacho.

Tabora iliiduwaza Azam kwa kuikung’uta mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, huku mabao yote ya wenyeji yakitokana na makosa ya kipa wa Azam, Mohamed Mustafa aliyetoka bila hesabu nzuri na kujikuta akipishana na mpira wa kichwa cha Heritier Makambo kabla ya kujifunga tena wakati akiokoa krosi ya Makambo aliyekuwa kwenye fomu nzuri katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara.

Kocha Anicet aliyejiunga na timu hiyo hivi karibuni kuchukua nafasi ya Mkenya Francis Kimanzi, alisema sio kwamba makosa ya Mustafa ndiyo yaliyoibeba timu hiyo iliyoendeleza ubabe kwa vigogo baada ya awali kuifunga Yanga kwa mabao 3-1, isipokuwa uwezo na ubora wa kikosi hicho kilichovuna pointi 24 kwa sasa.

“Ushindi wetu haujasababishwa na makosa ya kipa wao, isipokuwa ni ubora na nidhamu nzuri ya wachezaji kuanzia namna bora ya kujilinda na kushambulia, siri kubwa ni muunganiko mzuri kwao na umoja waliokuwa nao tangu nimewasili hapa,” alisema Anicet.

Kocha huyo aliongeza, Tabora inapaswa kupewa pongezi zaidi kutokana na mwenendo mzuri inayoendelea kuonyesha hadi sasa na si kuanza kuangalia udhaifu wa upande mmoja, kwani kwa kufanya hivyo ni kuwavunjia heshima jambo linalomkera kama kocha wa Nyuki wa Tabora.

Anicet aliyewahi kuzifundisha AS Vita Club, FC Simba Kolwezi, FC Les Aigles du Congo na Maniema Union, tangu ajiunge na kikosi hicho Novemba 2, mwaka huu hajawahi kupoteza mchezo wa Ligi Kuu na ipo nafasi ya tano kwa sasa baada ya mechi 14.

Kocha huyo tangu ajiunge na Tabora ameiongoza katika michezo mitano, akishinda minne na kutoka sare mmoja dhidi ya Singida Black Stars inayoshika nafasi ya nne kwa sasa ikiwa na pointi 27 sawa na ilizonazo Yanga, japo zinatofautiana idadi ya mechi ilizocheza na kileleni inaendelea kusalia Azam FC yenye pointi 30 na Simba ikishika nafasi ya pili kwa alama 28.

Related Posts