Kocha Azam amzuia Feisal | Mwanaspoti

AZAM FC jana jioni ilikuwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kumenyana na Tabora United katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku nyuma kocha wa kikosi hicho, Rachid Taoussi ametoa msimamo wake kwa kiungo mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Fei Toto anayeichezea Azam kwa msimu wa pili mfululizo sasa baada ya kuondoka kwa lazima katika kikosi cha Yanga, amekuwa mhimili wa timu hiyo kwa sasa ambapo kabla ya mechi ya jana alikuwa akichuana na nyota wa Simba, Jean Ahoua kwa kuhusika na mabao mengi (9), huku kukiwa na tetesi anaviziwa na Simba.

Taarifa za kiungo huyo kutakiwa na Simba, zimemfanya kocha Taoussi kutoa msimamo wake kwa kumzuia nyota huyo kuondoka Chamazi, kwa madai kwamba bado anahitajika na kikosi hicho kinachoutafuta ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya pili baada ya kutwaa mara ya kwanza msimuwa 2013-14.

Inaelezwa kwa sasa Fei Toto ameigomea klabu hiyo kuongeza mkataba mpya, huku ikidaiwa yupo kwenye mawindo ya Simba, lakini kocha Taoussi amesisitiza hapendi kuona kiungo mshambuliaji huyo anaondoka.

Fei alisaini mkataba wa miaka mitatu alipotua Azam na msimu wa kwanza alimaliza akiwa na mabao 19 na asisti saba akiwa nyuma ya Stephane Aziz KI aliyefunga mabao 21 na asisti nane, huku matajiri hao wa Chamazi wakimaliza katika nafasi ya pili na kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa walikotolewa raundi ya kwanza na APR.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya Azam zinasema kuwa, mabosi wa klabu hiyo wamekwama kumshawishi Fei Toto kusaini mkataba mpya wakati ule alionao ukiwa umesaliwa na muda wa mwaka mmoja tu ili kuweza kuwa huru na kuondoka kirahisi.

“Fei mkataba wake unakwisha 2026, lakini amewaambia mabosi wa Azam wasubiri kwanza msimu huu umalizike ndio afanye uamuzi,” kilisema chanzo hicho kutoka Azam, lakini akizungumza na Mwanaspoti kocha Taoussi, alisema bado anamhitaji mchezaji huyo aliyemsifia kuwa ana ushindani na mbunifu.

“Kama Fei ataendelea kusalia Azam nitapata utulivu mkubwa wa kuendeleza kiwango chake bora, kwani ana mchango mkubwa ndani ya timu,” alisema Taoussi.

Kabla ya mechi ya jana, Fei alikuwa na mabao manne na asisti tano, akichuana na Ahoua wa Simba aliyefunga mabao matano na asisti nne, wakiwa ndio wachezaji waliohusika na mabao mengi zaidi (9) kweye Ligi Kuu Bara kufikia sasa msimu huu wa 2024-25.

Related Posts