Walimu Mara watilia shaka agizo la RC ukarabati wa shule

Musoma. Baadhi ya walimu wa shule za Serikali mkoani Mara wameiomba Serikali kuharakisha ukarabati wa majengo ya shule yaliyoharibika kabla ya shule kufunguliwa Januari mwaka ujao. Walimu hao wameeleza wasiwasi wao juu ya usalama wa wanafunzi na walimu wanaotumia majengo hayo, ambayo yanadaiwa kuwa katika hali mbaya na kuhatarisha maisha.

Walimu hao wametoa maoni yao leo Jumamosi, Desemba 14, 2024, wakati wa mahojiano na Mwananchi Digital, baada ya agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi.

Mtambi amewataka wakurugenzi wa halmashauri kufanya tathmini ya majengo ya shule yaliyoharibika na kuandaa mpango wa ukarabati ndani ya siku 14.

Walimu hao ambao hawakutaka kunukuliwa wakisema si wasemaji, wamesema hali ya majengo mengi ni ya kusikitisha, huku baadhi yao yakitumiwa licha ya kuwa hayastahili kutumiwa na binadamu.

“Ninamshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuona umuhimu wa suala hili, lakini naomba ukarabati ufanyike kabla shule kufunguliwa. Hali ya sasa inapunguza morali yetu ya kazi,” amesema mmoja wa walimu hao.

Mwalimu mwingine amesema wanaingiwa na hofu ya majengo hayo kubomoka hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha kwenye baadhi ya maeneo.

“Hadi sasa hatujapata ajali, lakini kama hali itaendelea hivi, ipo siku mambo mabaya yatatokea japo hatuombei,” amesema mwalimu huyo.

Jengo lenye madarasa matatu katika Shule ya Msingi Mkiringo katika Wilaya ya Butiama likiwa limeezuliwa na upepo, shule hii ni miongoni mwa shule kongwe mkoani Mara zinazodaiwa kuwa na majengo chakavu. Picha na Beldina Nyakeke

Walimu hao pia wamesema tathmini ya hali ya majengo mara nyingi imekuwa ikifanyika, lakini utekelezaji wa ukarabati umekuwa wa kusuasua. Wamesema kuna majengo yenye nyufa kubwa, kuta zilizochakaa na mabati yaliyojaa kutu na mengine yameng’oka kabisa.

Changamoto hizo zipo mijini na vijijini na hali hiyo imeendelea licha ya fedha za ukarabati kupatikana.

Wakazi wa Musoma pia wamesema kuna shule zenye hali mbaya ambazo zinahitaji ukarabati wa haraka.

Gibai Wilson, mmoja wa wakazi hao amesema; “Kuna shule ukiziona huwezi kuamini kuwa ni za Serikali. Mkuu wa Mkoa atembelee shule hizo ajionee mwenyewe hali halisi.”

Naye Selina Mahende amesema baadhi ya madarasa yanayotumika hayana tofauti na magofu.

“Hali ni mbaya sana katika shule fulani. Agizo la Mkuu wa Mkoa linapaswa kufanyiwa kazi mara moja,” amesema.

Katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika Desemba 12, 2024, Mtambi alitoa siku 14 kwa wakurugenzi wa halmashauri zote tisa za mkoa huo kufanya tathmini na kuwasilisha mpango wa ukarabati wa shule kongwe, ambazo zinasemekana kuwa katika hali mbaya zaidi.

Mtambi alisema: “Ni wajibu wa wakurugenzi kuhakikisha mazingira ya shule ni salama muda wote. Serikali haitaendelea kuona wanafunzi wanasoma katika mazingira hatarishi wakati fedha za ukarabati zipo. Ni lazima tupate suluhisho la kudumu.”

Aliongeza kuwa ziara zake katika halmashauri mbalimbali zimemwezesha kubaini tatizo hilo, na akasisitiza kuwa hali ya uchakavu wa shule ni kikwazo kikubwa kwa usalama wa wanafunzi na walimu.

Related Posts