KOCHA wa KMC, Kally Ongala, amesema anahitaji kufanya kazi kubwa ili kuhakikisha kikosi chake kinapata makali ya kutosha na kufanya vizuri katika michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara, huku akitaka eneo la ushambuliaji analoendelea nayo kuliweka sawa.
Kally alikiri kwamba timu yake inahitaji kuboresha baadhi ya maeneo, hasa katika safu ya ushambuliaji, ili kufikia malengo ya kumaliza ligi katika nafasi nzuri.
Kocha huyo alisema kuwa anafurahi kuona mwanga wa maendeleo katika safu ya ulinzi, lakini alikiri kwamba bado kuna changamoto kubwa mbele yao, hasa kwa washambuliaji wa timu. Kally alieleza kuwa ni jambo la kusikitisha kwa timu kuwa na mechi nne na kufunga bao moja tu, na kwamba inahitaji kuboreshwa kwa haraka ili kuweza kushindana na timu nyingine.
Katika mechi hizo nne, KMC walipoteza dhidi ya Dodoma Jiji kwa mabao 2-1, na kupata matokeo ya kutofungana dhidi ya Mashujaa (0-0), huku wakifungwa na Simba (4-0) na Tabora United (2-0). Pamoja na kuonyesha kujitahidi, matokeo hayo yamekuwa na maumivu kwa kocha na wachezaji wa KMC, hasa ikizingatiwa kuwa walikuwa wakicheza nyumbani katika mechi ya juzi dhidi ya Mashujaa.
Akizungumza kuhusu mchezo dhidi ya Mashujaa, Kally alisema alifurahi kuona kikosi chake kilikuwa na ufanisi katika kujenga mashambulizi kutoka nyuma, lakini changamoto kuu ilikuwa ni kutokuwa na umakini na ufanisi katika eneo la mwisho.
“Tunapofika katika eneo la mwisho la uwanja, tunakutana na changamoto kubwa. Tunahitaji kuboresha umaliziaji na ufanisi wa washambuliaji wetu,” alisema Kally, nyota wa zamani wa Abajalo, Yanga na Azam.
Kocha huyo wa zamani wa Azam, alisema katika mazoezi wanajitahidi kufanya marekebisho, hasa kwa washambuliaji, na alisisitiza kuwa ushirikiano bora kati ya viungo na washambuliaji utakuwa na umuhimu mkubwa katika michezo ijayo.
Alikubali kuwa wakati mwingine ni vigumu kutengeneza nafasi za kufunga, lakini alijivunia juhudi za timu yake katika kujenga mashambulizi.