Maswa. Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge ametoa agizo la kuondolewa kwa Grace Tungaraza, Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) wilayani humo.
Hatua hiyo inatokana na madai ya kushindwa kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika wilaya hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya katoa agizo hilo leo Jumamosi Desemba 14, 2024 akiwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya, walipofanya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na Tasaf.
Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati na nyumba ya mganga katika kijiji cha Mbaragane, kwa gharama ya Sh92.4 milioni na ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Badi, unaofadhiliwa kwa Sh160.5 milioni.
Kwa mujibu wa Kaminyoge, fedha za miradi hiyo zilipokelewa tangu Mei, lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua.
Amesema hali hiyo imezua maswali kuhusu usimamizi wa rasilimali na uwajibikaji wa viongozi husika.
“Fedha za miradi ya zahanati na bweni la wasichana zipo kwenye akaunti ya halmashauri tangu mwezi wa tano, lakini hadi sasa ujenzi bado haujakamilika. Majengo ya zahanati yako hatua ya msingi na bweni liko kwenye usawa wa madirisha. Tulipanga kukamilisha miradi hii ifikapo tarehe 30 mwezi huu, lakini hali inasikitisha,” amesema Kaminyoge.
Amesisitiza wote waliohusika kukwamisha miradi hiyo, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Nimekuwa nikitoa elimu na maelekezo kila mara, lakini sasa nimefikia kikomo. Natangaza kuondolewa kwa mratibu wa Tasaf na ofisa ufuatiliaji. Tunahitaji watu watakaoweza kusimamia miradi hii kikamilifu,” amesema mkuu huyo wa wilaya.
Amesema wale watakaoteuliwa kuchukua nafasi hizo wahakikishe miradi inakamilika kwa wakati.
Akizungumza baada ya agizo hilo, Grace Tungaraza amesema licha ya juhudi za kusimamia miradi ya ujenzi, changamoto kubwa imekuwa ni wananchi kushindwa kuchangia sehemu yao ya rasilimali.
“Wananchi wanatakiwa kuchangia asilimia 10 ya gharama za miradi, ikiwa ni pamoja na kuleta mchanga, mawe, maji na kokoto. Lakini baadhi ya viongozi wa vijiji na kata wameshindwa kuwahimiza na kuwahamasisha wananchi kutimiza wajibu wao,” amesema Tungaraza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tasaf wilayani humo, Shedrack Mziray akizungumza na Mwananchi amesema agizo alilolitoa mkuu wa wilaya ni sahihi.
“Mkuu wa Wilaya ya Maswa ni kiongozi mahiri na mzalendo. Agizo lake tutalifanyia kazi mara moja. Pia nawatahadharisha watumishi wote wa Tasaf kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa bidii ili kufanikisha malengo ya kuwahudumia wananchi,” amesema Mziray.
Miradi ya maendeleo kama hii inategemewa kuboresha huduma za jamii, lakini utekelezaji wake unahitaji uwajibikaji wa hali ya juu ili kufanikisha lengo hilo.