Dar es Salaam. Kamati Kuu cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imekutana leo katika kipindi ambacho kuna joto la uchaguzi wa viongozi wa kitaifa ndani ya chama hicho, jambo ambalo linaonekana kuwagawa wanachama wake.
Kikao hicho cha Kamati Kuu kimefanyika Desemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam kikiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe.
Ajenda kuu za kikao hicho kwa mujibu wa John Mrema, mkurugenzi wa mawasiliano, itifaki na mambo ya nje, ni usaili na uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kanda za Kaskazini na Kati na maandalizi ya mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama ngazi ya Taifa.
Mbali na Mwenyekiti Mbowe, wajumbe wengine walioshiriki kwa mujibu wa picha zilizosambazwa na chama hicho ni Tundu Lissu (makamu mwenyekiti –Bara), John Mnyika (katibu mkuu) na Benson Kigaila (naibu katibu mkuu – Bara) na wengine.
Chama hicho kinaendelea na uchaguzi katika ngazi mbalimbali za uongozi kwenye kanda ambapo hadi sasa, tayari uchaguzi umefanyika kwenye kanda nane kati ya 10, hivyo zimebaki mbili ambazo wagombea wake wamesailiwa kwenye kikao hicho cha kamati kuu.
Baada ya kukamilika uchaguzi wa kanda, utafuata uchaguzi ngazi ya Taifa na moja ya ajenda za Kamati Kuu ni pamoja na kujadili maandalizi ya mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka 2025.
Mkutano huo utahudhuriwa na wajumbe zaidi ya 1,200 ambao watakuwa na kazi ya kumchagua uongozi wa taifa kwa miaka mitano ijayo.
Tayari Lissu ametangaza nia ya kugombea nafasi ya mwenyekiti kwenye uchaguzi huo akitaja malengo yake kuwa ni pamoja na kurudisha utaratibu wa kikatiba wa ukomo wa madaraka na kusimamia mifumo ya kifedha ya chama.
Uamuzi wa Lissu kuwania nafasi hiyo ya juu ndani ya chama, umeibua mjadala miongo mwa wanachama wa Chadema ambapo baadhi yao wanamuunga mkono Mbowe, wakitaka aendelee kukiongoza chama hicho na wengine wanataka mabadiliko wakiamini Lissu anafaa katika hilo.
Kumekuwa na minyukano mikali mtandaoni ambao pande hizo mbili zimekuwa zikirushiana maneno, kila mmoja ukieleza namna kiongozi wanayemtaka ndiyo sahihi kukiongoza chama hicho.
Hata hivyo, bado Mbowe hajatangaza nia ya kutetea nafasi yake kwenye uchaguzi huo licha ya kuwa katiba ya Chadema inamruhusu. Duru za ndani zinaonyesha kwamba Mbowe, ambaye amekuwa mwenyekiti wa Chadema tangu mwaka 2000, atagombea tena nafasi hiyo.
“Sioni Mbowe akiondoka kwenye chama katika kipindi hiki. Tunapitia kwenye majaribu makubwa, hawezi kukiacha chama katika mazingira ambayo siyo salama kwa uhai wake. Mbowe ni mpiganaji kwelikweli,” amesema kada wa Chadema, Godwin Kanoni.
Mbali na vigogo hao wawili, pia, wanaharakati wa haki za binadamu, Odero Charles Odero ametangaza nia ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa Chadema Taifa.
Novemba 23, 2024, Odero alisema tayari ameandika barua kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema kuhusu azma yake hiyo, na kuwa ameamua kugombea kwa lengo la kuimarisha demokrasia, mshikamano na maendeleo ya taifa.
Bado nafasi ziko wazi kwa mwanachama yeyote mwenye dhamira ya kuwania uenyekiti wa Chadema kutangaza nia yake.