Matukio ya mauji, ukatili yalivyoitikisa Zanzibar 

Unguja. Wakati tukielekea kuuaga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka 2025, matukio ya mauaji, kutekwa watu na ukatili wa kijinsia ni miongoni mwa mambo yatakayokumbukwa kwa namna ya pekee kisiwani hapa, miongoni mwa mengine.

Kati ya matukio hayo yamo ya watu wanaodaiwa kutekwa na kukutwa wameuawa kikatili, miili kuokotwa barabarani ikiwa imeharibiwa na ugonvi wa wanandoa na watoto kubwa kisha kuuawa.

Matukio hayo yametokea kuanzia Januari hadi Oktoba 2024 na Jeshi la Polisi limekiri ni matukio makubwa yanayosikitisha katika mikoa ya yote ya Zanzibar.

Wakati matukio hayo yakiripotiwa, baadhi ya ndugu wametaka uchunguzi wa kina ufanyike kubaini waliotenda uhalifu huo ili hatua zichukuliwe kuondoa hofu kwa wengine. 

Hata hivyo, kimyaa kinachoendelea kwa Jeshi la Polisi bila kutoa taarifa za uchunguzi licha ya ahadi zilizotolewa wakati wa matukio hayo ,ni jambo lingine linaloibua sintofahamu kwa ndugu wa waathirika na wananchi kwa ujumla.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Mchomvu licha ya kukiri kuwepo matukio hayo, anasema mengi bado yapo kwenye upelelezi.

Ali Bakari Ali, aliyekuwa katibu wa Chama Cha ACT-Wazalendo Jimbo la Chaani Mkoa wa Kaskazini, alitekwa na kuchambuliwa Machi mwaka huu na mwili wake kutelekezwa, alipoteza maisha akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mnazimmoja.

Pia, Mwananchi liliripoti tukio la Ramadhani Iddi Shaaban (48), mkazi wa Chumbuni ambaye alichukuliwa na watu waliojitambulisha ni askari wa vikosi vya SMZ wakidai wanampeleka Kituo cha Polisi Mwanakwerekwe kwa ajili ya mahojiano, lakini mwili wake uliokotwa siku inayofuata katika pori la Kijichi Spice Farm.

Watu hao walimchukua katika baa za Amani Mkoa wa Mjini Magharibi Septemba 24 saa 12:00 jioni.

Uchunguzi wa awali kwa mujibu wa polisi, ulibaini kifo chake kilitokana na kushambuliwa na vitu vyenye ncha kali na kusababisha majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake na kwa mujibu wa polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, uchunguzi bado unaendelea. 

Mama mzazi wa Ramadhani, Saada Ramadhani Mwendwa anaeleza jinsi familia yake inavyopata wasiwasi kutokana na kifo cha mwanaye.

“Siku hiyo mwanangu alienda kutembea jioni eneo la Amani baa, saa 12:00 jioni walikuja vijana watano wakamfuata alipokuwa amekaa na kumuita kwa jina, wakasema wana shida naye waende nje wakazungumze wakidai wao ni askari wa vikosi vya SMZ wana RB wanamtafuta.” 

Tukio lingine lilitokea Kisakasaka Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi, ambako mwili wa Kambalagula Mabula Chungwa (45) mkazi wa Fuoni Kibondeni ulipatikana ukiwa umetelekezwa pembezoni mwa barabara ukiwa na majeraha yaliyosababishwa na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, baada ya uchunguzi kina waliwakamata watuhumiwa watatu akiwemo mwanamke, Wile Dotto Ndombe (28) mkazi wa Kisakasaka aliyekamatwa Kimanzichana Mkoa wa Pwani na wengine wawili waliokamatwa Zanzibar. 

Oktoba 2, 2024 Masaka Juma Masaka maarufu Zahoro (40) mkazi wa Kijichi Nguruweni alimshambulia mkewe Zaituni Elias Kahindi kwa kumpiga na mchi kichwani na kusabaisha kifo chake, chanzo cha tukio ni ugomvi miongoni mwa wanandoa hao.

Hata hivyo, Mashaka naye anadaiwa kujinyonga Oktoba 3, 2024 kwa kutumia kamba aliyofunga kwenye mti wa mfenesi.

Katika tukio lingine ni la Askari wa Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ), Haji Machano Mohamed ambaye mwili wake uliokotwa Septemba kwenye msitu ukiwa umeharibika.

Hata hivyo, kilichosaidia kumbaini ni kutokana na nguo alizokuwa amevaa na simu yake iliyokutwa mfukoni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Daniel Shillah Septemba 28, askari huyo alipotea Agosti 8, 2024 alipokuwa na akiwa na wenzake katika mafunzo ya uongozi katika Chuo cha Uongozi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) Dunga.

 Tukio lingine la Novemba 9, 2024 ni lile watu wawili walipoteza maisha wakidaiwa kupigwa risasa na polisi kwa kosa la kukutwa na mchanga, huku wanafunzi wawili shule ya Msingi Kidoti wakijeruhiwa.

Waliofariki katika tukio hilo ni Msina Sharif (39) na msaidizi wake Abdala Bakari (28). Waliojeruhiwa ni Mohamed Issa (10) na Hamza Abdalla Abasi (10). 

Katika tukio hilo polisi kupitia Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai Zanzibar, Zubeir Chembera alisema wameunda kamati kuchunguza tukio hilo, hata hivyo kamati hiyo haijatoa matokeo ya uchunguzi wake.

 Katika tukio lingine la Septemba 20, 2024 ambapo, Idarous Masoud Omar (23), mkazi wa Tomondo aliuawa saa 11:00 alfajiri maeneo ya Mombasa Wilaya ya Magharibi B.

Hata hivyo, katika tukio hilo polisi imeeleza kuwakamata waliofanya unyama huo ambao ni Hassan Hafidh Juma maarufu Mwarabu (23) wa Melinne na Yunus Issa Nassor (28) wa Nyarugusu.

Marehemu alituhumiwa kwa kosa la wizi wa pikipiki, ikidaiwa akiwa na wenzake walifanya unyang’anyi wa pikipiki na mmiliki wa pikipiki hiyo alipiga kelele kuomba msaada kwa wananchi,” amesema. 

Msemaji wa ofisi, Kamati ya Wasemaji wa Kisekta, ACT -Wazalendo Zanzibar, Hamad Mussa Yussuf amesema matukio ya mauaji yanalitia doa Taifa huku kukiwa hakuna hatua thabiti zinazochukuliwa.

“Matukio kama haya ya mauaji yaliyotokea hivi karibuni mengine kuhusisha vyombo vya dola hayaoneshi taswira njema kwa nchi na yanatia wasiwasi na mashaka kwa wananchi wa Zanzibar,” amesema.

Amesema ipo haja kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wanakomesha vitendo hivyo hata wanaohusika wanakamatwa ili kuleta imani kwa wananchi. 

Pamoja na hatua hizo, amesema msimamo wa chama hicho ni kulifanyia Jeshi la Polisi mabadiliko ya kiutendaji na kimfumo ili kuleta uwajibikaji.

Mwanaharakati wa haki za binadamu, Khairat Haji amesema ipo haja vyombo vya dola kuyadhibiti kwani yanaleta taharuki kwa wananchi na taswira mbaya kisiwani humo.

“Haya matukio yanatufanya tuage mwaka kwa kumbukumbu tofauti tulikuwa tunayasikia maeneo mengine, ila inaonekana hata huku yametikisa, hii sio dalilia njema,” amesema Khairat Haji mkazi wa Ziwani.

Mkazi mwingine Yunes Kitarao amesema “tunaamini vyombo vya dola havishindwi kuwabaini wanaotenda makosa hayo kwani vina mbinu nyingi kuhakikisha waliotenda wanabainika na hatua zichukuliwe za wazi ili liwe fundisho kwa wengine.”

Licha ya jitihada zinazochukuliwa na serikali, mashirika, taasisi na wanaharakati wa kupinga udhalilishaji Zanzibar, bado vitendo hivyo vimeendelea kushamiri kwa namna yake kisiwani hapa mwaka huu.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, matukio ya ukatili na udhalilishaji yamekuwa yakipungua na kuongezeka kati ya mwezi mmoja na mwingine.

Taarifa ya ofisi hiyo, kwa kipindi cha Januari hadi Oktoba mwaka huu, jumla ya matukio 1,585 yameripotiwa huku yale ya watoto yakichukua asilimia kubwa ikilinganishwa na wanawake na wanaume. 

Kati ya kesi hizo, 1,337 zinahusisha watoto (wa kike 1,095 na wa kiume 242. Na kati ya kesi hizo zilizofikishwa mahakamani ni 74, huku kesi 1,153 zipo kwenye uchunguzi na 341 zipo kwa Mkurugenzi wa Mashataka (DPP).

Hakimu katika mahakama ya udhalilishaji, Nayla Abdulbast amesema bado kuna usiri mkubwa kwa familia, hivyo wazazi wanatakiwa kuwaeleza ukweli watoto na kwamba kesi nyingi zinakosa msingi wa ushahidi.

Mchungaji Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Shukuru Maloda amesema bado kuna kazi ya kufanya kwa viongozi wa dini kushirikiana na jamii kufundisha maadili na watu kuwa na hofu ya Mungu.

Mkuu wa dawati la jinsia la Jeshi la Polisi, Rahima Ali Salum amesema bado kuna changamoto ya muhali huku baadhi ya wazazi wakubaliana kufuta kesi, hivyo lazima jamii ibadilike ili kufanikiwa. 

“Kwahiyo bado kazi ipo lakini jamii haijakubali kubadilika kesi zinakufa kwa sababu watu wanaelewana wakati mwingine watuhumiwa wanabadilishwa, sasa hapa lazima tushirikiane, kila mmoja kwa nafasi yake atimize wajibu wake.

Related Posts