MASHABIKI wa Yanga wamegawanyika kimtindo kwa sasa juu ya usajili wa beki mpya wa kulia Israel Mwenda aliyesajiliwa kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, lakini kuna kocha mmoja wa zamani wa watani wa jadi, Simba amewatumia salamu Wananchi hao.
Mwenda ametambulishwa katikati ya wiki hii na muda mfupi baadae aliibukia mazoezini sambamba na kikosi hicho kabla hakijaondoka kwenda DR Congo kuwahi mchezo wa jana wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya TP Mazembe, huku mashabiki wa klabu hiyo wakigawanyika wakiona hawezi kuwa na maajabu.
Sababu ya kugawanyika huko ni kwa vile kikosi wana mabeki wa pembeni wanne wanaoonekana ni wakali zaidi akiwamo Yao Kouassi na Kibwana Shomari wanaocheza kulia na Chadrack Boka na Nickson Kibabage wanacheza kushoto mbali na Dickson Job na Denis Nkane wanatumika pia eneo na kulia kunapotokea tatizo.
Hata hivyo, kocha wa zamani wa Simba ambaye kwa sasa yupo Rwanda akiinoa Rayon Sports, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, amekuwa akifuatilia kila kitu kinachoendelea nchini na kukiri kwa usajili wa Mwenda Yanga imelamba karata dume, kwani ni mchezaji mzuri atakayewafanyia makubwa kama watamuamini.
Robertinho aliyefanya kazi na Mwenda wakati wakiwa wote Simba, alisema Yanga itanufaika na Mwenda kutokana na bado kijana mdogo ana nishati ya kutosha.
Robertinho aliongeza, Yanga pia imepata beki sahihi atakayempa presha Yao Kouassi ambaye naye ni beki mwenye nishati kubwa.
“Ni usajili mzuri kwa Yanga namjua vizuri Israel (Mwenda) nishati yake ni kubwa sana uwanjani, anaweza kutumika kwa nguvu kwa kuwa bado kijana mdogo mwenye kiu ya mafanikio,” alisema Robertinho aliyetimuliwa mara baada ya Simba kufumuliwa mabao 5-1 na Yanga katika Dabi ya Kariakoo iliyocheza Novemba 5 mwaka jana, aliyeongeza;
“Katika timu unatakiwa kuwa na watu wawili bora kila nafasi ili washindane kutafuta nafasi, nadhani kule kulia kwa Yanga watakuwa na Yao ni mzuri sana, lakini Israel ni mzuri na atamfanya Yao ajitume zaidi.”
Kocha huyo mwenye uraia wa Brazili, alisema anajua sababu kwa nini Mwenda alishindwa kucheza vizuri Simba na hakuona kama angeweza kudumu ndani ya timu hiyo, huku akificha kueleza siri hiyo.
“Nafahamu kwa nini ilikuwa ngumu Israel kubaki kwa muda mrefu ndani ya Simba, kulikuwa na mambo ambayo yalihitaji sana akili kubwa kuyaweka sawa ambayo sitaki kuyaweka wazi kwako lakini hayakuharibu kipaji chake kwa kuwa ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa,” alisema Robetihno na kuongeza;
“Israel ni beki ambaye unaweza kumtumia kwenye mifumo mingi tofauti kutokana na utayari wake wa kubadilika, kuna aina ya soka ambalo nimeona Yanga wanajaribu kulitumia nadhani atawasaidia sana.”
Mwenda aliyetambulishwa katika Ligi Kuu na Alliance kabla ya kusajiliwa Simba na baadae Singida anasifika kwa kumudu kucheza beki zote za pembeni na eneo la winga zote, nafasi ambazo ndani ya Yanga zina watu.